Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville (kushoto).
Askofu Blaston Gaville wakati akiwekwa wakfu kuongoza Dayosisi ya Iringa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
KUKAMILIKA kwa mchakato wa uaandaaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutasaidia kuweka misingi imara na kuondoa changamoto zilizopo katika Katiba ya sasa, hivyo kukomesha ufisadi na kuinua uchumi wa Tanzania.
Aidha, kukamilika huko kwa Katiba Mpya kutaakisi jitihada kubwa
zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.
zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT) Dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville, ambaye alimtaka Rais Magufuli kuumalizia
mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya, kwani alisema mbali ya kuakisi kasi yake
anayoifanya ya kukuza uchumi pia kutasaidia kuhimiza uwajibikaji.
“Wakristo na Watanzania kwa ujumla tuna imani kubwa na
Serikali ya Awamu ya Tano na ni matarajio yetu kwamba mchakato wa kuandika
Katiba utamalizwa kama lengo lilivyokuwa,” alisema.
Askofu Gaville amesimikwa ili kuchukua nafasi ya Askofu Dkt.
Owdenburg Mdegella ambaye amestaafu.
Alisema wanatiwa moyo na jitihada zinazoendelea kufanywa na
Dkt. Magufuli katika kufufua uchumi na kuhakikisha rasilimali za nchi
zinatumika kwa manufaa ya Watanzania wote.
Alisema Tanzania ina wanyonge wengi kuliko wenye nguvu, hivyo
wanatiwa moyo na jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli na serikali yake hasa
anapowatetea wanyonge.
Aidha, pamoja na kupongeza jitihada hizo, Askofu Gaville, aliishukuru
Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa kodi akisema
hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo bila mapato hayo.
“Tunaiomba serikali iangalie upya suala la kodi kwa
mashirika ya dini kwani baadhi ya kodi tunazolipa, ikiwemo ya kuendeleza vyuo
vya ufundi na ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, zimekuwa mzigo mkubwa kwaetu.
“Kazi ya Kanisa ni kutoa huduma, siyo kutengeneza faida,
kodi hizo zimeleta changamoto kubwa kwa uendeshaji wa taasisi, tunaomba
serikali iziangalie upya,” alisema.
Kuhusu elimu, Askofu Gaville alisema Kanisa linasaidia watoto
maskini ili wapate haki yao ya elimu na akaiomba serikali isiwaingize katika
kundi la watoto wanaotoka katika familia zenye uwezo kwa sababu wanasoma shule
binafsi.
“Wanapojiunga na vyuo vikuu, tunaomba Bodi ya Mikopo
isiwanyime mikopo stahiki kwa kisingizio cha shule wanazotoka, ufanyike
upembuzi ili kutoa msaada kwa walengwa wote,” alisema.
Aidha, alisema Dayosisi ya Iringa inatoa mwaliko kwa vyama
vyote vya kisiasa na jamii nzima ya Watanzania kuendeleza na kukuza tunu ya
ushirikiano na moyo wa kizalendo ili kuwa na maendeleo yenye tija, badala ya
kujenga uhasama kwa sababu za kiitikadi.
Katika salamu zake kwa waumini wa dayosisi hiyo, Askofu Mkuu
wa KKKT Tanzania, Dkt. Fredrick Shoo, alizipongeza kamati mbili za madini
zilizoundwa na Rais Magufuli akisema zimewaumbua baadhi ya Watanzania
waliodhani ni sifa kusaini mikataba ya madini inayonyonya haki ya Watanzania.
“Kama hao watu waliosaini hiyo mikataba walidhani wanaisadia
nchi huku wakijua mikataba hiyo inalenga kuiibia nchi, wajue hayo ni mambo ya
aibu na ni upumbavu mkubwa kufanya mambo kama hayo kwa ajili ya matumbo yao
binafsi,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William, akitoa salamu
za serikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, alisema
serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zote za dini ili kufikia malengo
yake ya maendeleo.
William alizungumzia fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo
mkoani Iringa na akawaomba Watanzania na wawekezaji kuzitumia ipasavyo kuunga
mkono jitihada za Rais za kuifanya nchi kuwa ya viwanda.
Katika hatua nyingine, Askofu Mstaafu wa Dayosisi hiyo, Dkt.
Owdenburg Mdegela, aliipongeza serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa hatua
mbalimbali inazochukua kujirekebisha.
Akiungana na mamia ya wakazi wa Mkoa wa Iringa katika
maandamano ya amani siku moja kabla ya kumsimika Askofu Gaville, Dkt. Mdegela
alisema moja ya makosa makubwa yaliyofanywa na serikali lilikuwa ni kuua Azimio
la Arusha la mwaka 1967.
Maandamano hayo yalifanyika mjini Iringa kwa nia ya
kupongeza juhudi zinazofanywa na Rais Dkt. Magufuli katika kushughulikia
changamoto zinazolikabili Taifa, ambapo yalipokelewa katika viwanja vya
Mwembetogwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, huku yakihudhuriwa na
viongozi mbalimbali wa dini, siasa na serikali, watumishi, wanafunzi, wafanyabiashara
na wadau wengine wa maendeleo kutoka wilaya zote za mkoa huo.
“Hatukupaswa kuua Azimio la Arusha pamoja na kwamba kuna
mambo yalipaswa kubadilishwa. Kimsingi azimio lile lilikuwa na mambo mengi ya
msingi ambayo ni ya faida kwa Taifa, hayo ni pamoja na maadili kwa viongozi na
msingi wa kujitegemea,” alisema.
Alibainisha wazi kwamba, serikali ya CCM ilichoka, lakini
kupitia kwa Rais Magufuli imeanza kujirekebisha ikiwa ni pamoja na kutembea
katika misingi ya Azimio la Arusha, hatua inayopaswa kupongezwa hadharani.
“Anayempinga Rais anayekamata wezi, watumishi hewa na
anayepambana kulinda rasilimali za nchi kwa manufaa ya Watanzania wote na
kuhimiza uwajibikaji lazima atakuwa alipata matokeo mabaya ya mtihani wa darasa
la saba na kidato cha nne.
“Tunapaswa kuiona falsafa ya kiongozi wetu pamoja na kwamba
wapo watu wanambeza kwa maneno mengi ya kuudhi lakini wanaombeza Magufuli
wakumbuke kwamba hata Mungu alibezwa na theluthi moja ya malaika zake,”
alisema.
Amina Masenza, katika utangulizi wake, alisema Ilani ya
Uchaguzi ya mwaka 2015 inasema katika miaka mitano ijayo, CCM itazielekeza
serikali zake kutumia nguvu zake zote kuondoa umaskini, kutatua tatizo la ajira
hasa kwa vijana, katika vita dhidi ya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma na
kudumisha amani, ulinzi na usalama.
No comments:
Post a Comment