Kufundisha Kwa Uhuru, Kuwawezesha Walimu
Walimu ni msingi mkuu katika ustawi wa muda mrefu wa kila jamii kwa kuwa hujishughulisha kuwapatia watoto, vijana na watu wazima elimu na ujuzi wanaohitaji ili kufikia uwezo wao.
Lakini duniani kote, walimu wengi sana hawana uhuru na msaada wanaohitaji kufanya kazi yao iliyo muhimu sana. Ndiyo maana maudhui ya Siku ya Walimu Duniani kwa mwaka huu – ‘'Kufundisha kwa Uhuru, Kuwawezesha Walimu'’ - inathibitisha thamani ya walimu waliowezeshwa na kutambua changamoto ambazo wengi hukabiliana nazo katika maisha yao ya kitaaluma ulimwenguni kote.
Kuwa mwalimu aliyewezeshwa ina maana ya kuwa na uwezo wa kupata mafunzo yenye ubora, malipo ya haki, na fursa zisizo na mwisho za kujiendeleza kitaaluma. Pia inamaanisha kuwa na uhuru wa kuunga mkono maendeleo ya mitaala kitaifa – na uhuru wa kitaaluma wa kuchagua njia sahihi na mbinu zinazofaa zaidi kuwezesha utoaji wa elimu yenye ufanisi, jumuishi na ya usawa. Zaidi ya hayo, inamaanisha kuwa na uwezo wa kufundisha kwa usalama wakati wa mabadiliko ya kisiasa, machafuko, na migogoro.
Lakini katika nchi nyingi, uhuru wa kitaaluma na uhuru wa mwalimu viko chini ya shinikizo. Kwa mfano, katika ngazi za shule za msingi na za sekondari katika baadhi ya nchi, mipango ya uwajibikaji imeweka shinikizo kubwa kwa shule kutoa matokeo kwa vipimo vilivyowekwa, na kupuuza haja ya kuhakikisha mtaala wa msingi unaofaa mahitaji tofauti tofauti ya wanafunzi.
Uhuru wa kitaaluma ni muhimu kwa walimu katika kila ngazi ya elimu, lakini ni muhimu zaidi kwa walimu wa elimu ya juu, ili uwawezeshe kutumi uwezo wao wa kuvumbua, kuchunguza, na kuendeleza utafiti kuhusiana na namnaza kisasa zaidi za kufundisha. Katika ngazi ya elimu ya juu, mara nyingi walimu hupatiwa mikataba ya ajira ya kipindi maalumu.
Hii inaweza kusababisha hali ya kutokuwa na uhakika wa ajira kwa walimu, kupungua kwa matarajio ya kukua kitaaluma, mzigo mkubwa wa kazi na malipo duni – yote haya yanaweza kuzuia uhuru wa kitaaluma na kudhoofisha ubora wa elimu ambayo walimu wanaweza kutoa.
Katika ngazi zote za elimu, shinikizo la kisiasa na maslahi ya kibiashara yanaweza kuzuia uwezo wa walimu kufundisha kwa uhuru. Waalimu wanaoishi na kufanya kazi katika nchi na jamii zilizoathiriwa na migogoro na machafuko mara nyingi hukabiliwa na changamoto kubwa zaidi, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa kuvumiliana, ubaguzi, na vikwazo vinavyohusiana na utafiti na kufundisha.
Mwaka huu unaadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 ya Mapendekezo ya UNESCO ya 1997 kuhusu Hali ya Wakufunzi wa Elimu ya Juu, ambayo inakamilisha Mapendekezo ya UNESCO / ILO ya 1966 kuhusu Hali ya Walimu. Kwa pamoja, vyombo hivi hufanya mfumo mkuu wa rejea juu ya haki na wajibu wa walimu na waelimishaji. Yote yanasisitiza umuhimu wa uhuru wa mwalimu na uhuru wa kitaaluma katika kujenga ulimwengu ambapo elimu na kujifunza ni kwa ajili ya wote.
Wakati dunia inapofanya kazi pamoja ili kufikia maono ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, tunawaomba washirika wetu katika serikali, sekta ya elimu na sekta binafsi kujitolea kubeba jukumu la kuwaandaa waelimishaji wenye ujuzi ulio bora zaidi, wenye thamani na waliowezeshwa.
Hii ni njia muhimu katika kuyafikia maono ya Malengo ya Maendeleo Endelevu hasa lengo namba 4 lenye nia ya kuwa na ulimwengu ambapo kila msichana, mvulana, mwanamke na mwanaume wanapata elimu bora na fursa za kujifunza katika maisha yao yote.
Hii inamaanisha kuwapatia walimu mazingira mazuri ya kazi na mishahara iliyo bora, ikiwa ni pamoja na walimu wa ngazi ya juu. Inamaanisha kuwapa walimu mafunzo na fursa ya kujiendeleza. Inamaanisha kuongeza idadi ya walimu wenye ubora, hasa katika nchi zenye idadi kubwa ya walimu na waelimishaji wasio na elimu ya kutosha.
Inamaanisha ya kuondoa vikwazo visivyo vya lazima katika utafiti na kufundisha na kulinda uhuru wa kitaaluma katika ngazi zote za elimu. Na mwisho, inamaanisha kuinua hadhiya walimu duniani kote kwa namna ambayo inaheshimu na inayoonyesha matokeo waliyonayo walimu katika jamii.
Katika Siku hii ya Walimu Duniani, ungana nasi katika kuwawezesha walimu kufundisha kwa uhuru ili kwamba, kila mtoto na kila mtu mzima awe huru kujifunza – kwa manufaa ya dunia iliyo bora zaidi.
Imetolewa na Irina Bokova, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO; Guy Ryder, Mkurugenzi Mkuu wa ILO; Anthony Lake, UNICEF Executive Director; Achim Steiner, UNDP Administrator; pamoja na Fred van Leeuwen, General Secretary of Education International.
No comments:
Post a Comment