Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Watu wawili wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiuguza majeraha ya risasi walizopigwa na polisi wakidaiwa kukaidi amri walipotakiwa kusimamisha gari walilokuwa wakiendesha.
Watu hao ambao walijeruhiwa juzi wametajwa kuwa ni Gasper Mlay na Gabriel Mauki waliokuwa katika gari aina ya Toyota Corolla eneo la Bwawani karibu na Kiluvya, Dar es Salaam wakielekea Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumzia tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema japo limetokea mkoani Pwani, analifahamu kwa kuwa lilihusisha pia na eneo lake.
“Walisimamishwa na askari Kibaha lakini hawakusimama ikabidi askari huyo achukue pikipiki kuwafuatilia lakini bado hawakutii amri,” alisema.
Kamanda Mambosasa alisema, “Askari alitoa taarifa na walianza kuzuiwa barabarani lakini walikuwa wanawatishia askari kuwagonga. Walikwenda mpaka njia panda ya Bagamoyo wakageuza na ndani ya gari kulikuwa na bia.”
Alisema kutokana na hali hiyo, polisi walilazimika kufyatua risasi hewani ili kuwatisha lakini bado waliendelea kutotii amri ndipo wakapiga risasi matairi ya gari.
“Mmoja alikwaruzwa na risasi begani na mwingine risasi ilimpata kwenye kisigino. Wapo wanatibiwa Muhimbili wakiwa chini ulinzi. Tunachunguza kujua tukio hilo ni la aina gani maana linaweza kuwa la ulevi na uhalifu,” alisema.
Akizungumza kwa simu jana jioni, Mlay aliyekuwa dereva wa gari hilo alisema walikuwa wakiwahi Kibaha kuchukua nguo ili kuungana na wenzao kusafirisha mwili wa marehemu.
“Tulipita bila kusimama katika eneo ka wavuka kwa miguu pale Mbezi, mbele yetu kulikuwa na askari akatusimamisha. Nilisimama na kufungua kioo kisha nikamweleza kuwa tuna dharura tunawahi msiba, baada ya kumueleza hayo nikaondoa gari bila kupata majibu yake,” alisema.
“Nilijua amenielewa lakini baadaye tulianza kufukuzwa na Defender ya polisi na tulipofika bwawani tulikuta vizuizi vya barabara na kabla sijasimama nilisikia tairi moja imepigwa risasi ikabidi nitulie.”
Mlay alisema baada ya kusimama katika kizuizi, gari lilishambuliwa kwa risasi.
“Sikumbuki idadi ya risasi, ila ninachokumbuka ni kutolewa katika gari mimi na kaka yangu na kupelekwa Muhimbili,” alisema.
Alisema walishangazwa na kitendo cha kushambuliwa kwa risasi bila kusikilizwa kwa madai kuwa gari lao halikuwa katika mwendo mkali kutokana na foleni kubwa katika Barabara ya Morogoro.
“Tupo hapa Muhimbili jengo la Kibasila wodi namba 11 , mpaka sasa tupo chini ya uangalizi wa polisi na mpelelezi amemaliza kunihoji,” alisema Mlay.
No comments:
Post a Comment