Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Kondoa Vijijini Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) akielezea maendeleo ya viwanda katika Halmashauri hiyo kwa kusisitiza kujikita katika kilimo ili kupata malighafi wakati wa Mkutano na viongozi wa Idara mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Bw. Falesy Mohamed Kibassa (wa pili kulia) akipongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Kondoa Vijijini Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) katika kufanikisha maendeleo ya Wilaya hiyo wakati wa Mkutano kati yake na viongozi wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Kondoa Vijijini Dkt. Ashatu Kijaji (kushoto) akizungumza jambo na Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Bi. Hilda Saganda (kulia) baada ya kumalizika kwa Mkutano kati ya Naibu Waziri huyo na viongozi wa idara katika Halmashauri hiyo. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango).
Na Benny Mwaipaja, Kondoa.
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma kutenga fedha kwenye bajeti ya Mwaka ujao wa Fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Kondoa ili kukabiliana na changamoto za afya zinazowakabili wananchi.
Dkt. Kijaji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini, ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa halmashauri ya Wilaya ya Kondoa wakati akianza ziara yake ya siku mbili wilayani humo kukagua shughuli za maendeleo zinazotokana na fedha zilizotolewa na Serikali ikiwemo ujenzi wa vituo vipya vya afya pamoja na miundombinu ya elimu wilayani humo.
Alisisitiza kuwa atafuatilia na kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa ili kusogeza huduma ya afya karibu zaidi na wananchi hususan waishio vijijini ambao wanakosa huduma ya uhakika kutokana na kukosekana kwa hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Kondoa.
Aidha, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amewataka watendaji wa halmashauri hiyo ya Wilaya ya Kondoa kuhakikisha kuwa wanawatumikia wananchi kwa moyo, umoja na mshikamano ili malengo ya kitaifa ya kuwaletea maendeleo kupitia dhana ya Tanzania ya viwanda yaweze kufikiwa.
Alisema kila idara, ikiwemo ya kilimo, maji, elimu, afya, maendeleo ya jamii na miundombinu ya barabara ihakikishe inatimiza malengo yake ili wananchi waongeze uzalishaji hususan sekta ya kilimo itakayochangia upatikanaji wa malighafi itakayotumika katika uzalishaji viwandani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wialaya ya Kondoa Bw. Falesy Mohamed Kibassa ameahidi kuwa Halmashauri yake imejipanga kuhakikisha kuwa malengo waliyojiwekea ya kuwatumikia wananchi wa Wilaya ya Kondoa yanafikiwa kwa kuimarisha usimamizi na utendaji kazi katika idara zote.
Alimhakikishia Dkt. Kijaji kwamba kwa kushirikiana kama timu moja kati yake na watendaji wake, watahakikisha wanaifikisha wilaya hiyo kwenye maendeleo yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment