ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 9, 2018

Mnara wa simu wajeruhi askari

JENGO la ofisi ya serikali ya mtaa katika eneo la Goba jijini Dar es Salaam ambalo hutumiwa na polisi, limeangukiwa na mnara wa simu kutokana na mvua iliyonyesha juzi usiku na kumjeruhi askari.
Mvua hiyo ambayo ilianza majira ya jioni ikiambatana na upepo mkali, ilisababishia mnara huo kuanguka na kumjeruhi askari ambaye alikuwa anatoa huduma kwa wananchi katika eneo hilo.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa eneo hilo linalotumika na askari sio jengo lao, bali ni mali ya ofisi ya serikali ya mtaa.
 
“Katika hilo eneo hatuna kituo cha polisi, ila polisi wetu wanakuwa wapo mobile kwa hiyo tukiwa kwenye majengo ya serikali ya mtaa tukiwa tunatoa huduma ina maana ni kituo cha polisi. Hivi kituo cha polisi kinakuwa na chumba kimoja ina maana ukipita sehemu ukaona polisi watatu hicho ni kituo cha polisi,” alihoji Kamanda Murilo.

Alifafanua kuwa wakati jengo hilo linaangukiwa na mnara kulikuwa na askari mmoja ambaye alikuwa anatoa huduma za kiusalama katika eneo la Goba na alipata majeraha kadhaa na hali yake inaendelea vizuri.
 
Alisema askari huyo alikwenda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na sasa yupo nyumbani akiendelea vizuri.

No comments: