ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 15, 2018

UNESCO wafunda ujasirimali Walimu kufundisha wanafunzi kujitambua

Walimu wanaopatiwa mafunzo ya siku nne ya ujasiriamali yanayotolewa na Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa(UNESCO) chini ya ufadhili wa program ya Malala wametakiwa kuhakikisha wanatumia elimu waliyopata kuwafanya wanafunzi hasa wa kike kujitambua na kukamilisha malengo yao. Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Elimu wa mkoa wa Tanga, Mayasa Hashimu wakati akifungua semina hiyo inayoshirikisha wajumbe 64 wakiwemo walimu 40 na wakuu wa Shule 20 na maofisa elimu wanne kutoka wilaya nne za mkoa wa Tanga. Wilaya zinazohusika ni za Pangani, Muheza, Korogwe na Lushoto. Semina hiyo ni sehemu ya mradi wa kuwafanya watoto hasa wa kike kujitambua, kupunguza utoro na mimba za utotoni ili kufikia malengo yao ulioanza mwaka 2015. Mayasa alisema kwamba ili wawasaidie watoto hao wamalize masomo yao ni vyema walimu hao wakatambua umuhimu wa mafunzo hayo na kuwa karibu na watoto na kuishi nao kutambua shida zao na kuwasaidia kukabiliana nazo ili waweze kusonga mbele. Alisema kama walimu wakiamua kufanyakazi ya kufundisha tu bila kuwa karibu na watoto dhima ya kuwasaidia kufikia malengo hata ya kujiajiri wenyewe wakimaliza masomo haitafikiwa. Aliwataka walimu hao kusogeza elimu yao kwa wenzao na katika hilo kuweza kusaidia kufanya vyema kwa watoto katika masomo na pia utayari wa maisha. Aliwakumbusha walimu kusikiliza watoto kutambua shida zao na kujua namna ya kuwasaidia badala ya kubaki kulalamika kwamba watoto hao ni wakorofi au wanakiuka kanuni za shule. Alisema alishawahi kutembelea shule moja na kukuta mtoto ambaye anachelewa kufika shule lakini alipohoji aligundua kwamba kijana huyo wa kidato cha nne ana mama mgonjwa mahututi na lazima amhudumie kwa kuwa baba yake alikwishafariki. “Walimu walimshambulia yule mtoto, nikamuita pembeni na kujua tatizo lake” alisema Ofisa Elimu huyo ambaye pia alisema alikutana na kadhia hiyo pia kwa binti mmoja ambaye alilazimika kusaidia kuhamishwa kwake kupata hosteli kutokana na mazingira magumu aliyomo. Aliwataka walimu wanaochukua mafunzo hayo kubadilisha mtazamo na kuacha kuchukulia kazi kimazoea ili hata wafadhili nao waone fahari ya mchango wao katika elimu. Alisema kwamba kuendelea kuwa na shule dhaifu wakati kuna wafadhili wanapiga jeki si sawasawa; aliwataka walimu waamke na kuhakikisha kwamba mafunzo wanayoyapata yanawaondoa wanafunzi katika dhiki ya kujitambua na kujipanga kufikia malengo. Alisema miongoni mwa mambo yanayostahili kuangaliwa ni pamoja na kuhakikisha klabu zilizoanzishwa zinasonga mbele na kutoa matunda tarajiwa ili wafadhili nao wasichoke. Pamoja na mafunzo hayo kutakiwa kufika kwa wanafunzi pia amewataka kuambukiza elimu yao kwa walimu wenzao ili kuwa na moyo mmoja wa kusaidia watoto hasa wa kike ambao wanakumbana na vishawsihi vingi. Aliwataka walimu wengine pia kuiga Mkuu wa shule ya Kalemea ambaye pamoja na kuwa pembezoni amekuwa karibu na watoto na kiasi cha kutoa divisheni ya kwanza katika wilaya yake ya Lushoto. Katika mafunzo hayo ambayo yaliendeshwa na Mkufunzi kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Ofisa Miradi wa UNESCO Jeniffer Kota alisema kwamba lengo la semina hiyo ya ujasiriamali ni kutoa elimu kwa walimu namna ya kuwawezesha watoto wa kike kujitambua hivyo kupunguza utoro, mimba za utotoni na kuongeza maarifa ili waweze kumaliza shule angalau elimu ya msingi. Alisema elimu hiyo inayotolewa kwa wakuu wa shule na walimu wengine na maofisa elimu wilaya ni kuona kwamba walimu hao wanawafunza wengine ili kupeleka elimu kwa watoto nao waelewe thamani ya elimu na kuwa na uwezo wa kutimiza malengo na kujiajiri. Naye mgeni kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, wa idara ya elimu Simon Mombeyi aliwatafadhalisha walimu wanaochukua mafunzo hayo kuyafikisha kwa walimu wengine na kufikisha elimu hiyo kwa wanafunzi.; Alisema kwa kuwa lengo la msingi ni kuwezesha wafikie malengo wanayofikiria kwa kuwawezesha kujitambua na kubaki katika mstari. Alisema wanafunzi wa sekondari wana vishawishi vingi kwa kuwa wanapanga hivyo wanapojengewa uwezo wanaweza kudhibiti mihemko ya ujana na kumaliza elimu kama ilivyopangwa. Alisema rais amewekeza katika elimu na wao wanamsaidia lakini wanatakiwa kuwekeza kwa busara sana ili kufanikisha malengo hayo.
Ofisa Mradi wa Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), Jennifer Kotta akitoa neno la ukaribisho kwa washiriki wa mafunzo ya siku nne ya ujasiriamali yanayotolewa na UNESCO chini ya ufadhili wa program ya Malala yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani Tanga.
Mgeni rasmi Ofisa Elimu wa mkoa wa Tanga, Mayasa Hashimu akitoa nasaha wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne ya ujasiriamali yanayotolewa na UNESCO chini ya ufadhili wa program ya Malala yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani Tanga. Kushoto ni Ofisa Mradi wa Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), Jennifer Kotta na kulia ni Simon Mombeyi kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, wa Idara ya Elimu.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya siku nne ya ujasiriamali yanayotolewa na UNESCO chini ya ufadhili wa program ya Malala wakisikiliza kwa umakini nasaha za mgeni rasmi (hayupo pichani) yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani Tanga.
Simon Mombeyi kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, wa Idara ya Elimu akizungumza jambo na washiriki wa mafunzo ya siku nne ya ujasiriamali yanayotolewa na UNESCO chini ya ufadhili wa program ya Malala yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani Tanga.
Mkufunzi wa mafunzo ya ujasiriamali kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Jacqueline Stenga akiendesha mafunzo ya siku nne ya ujasiriamali yanayotolewa na UNESCO chini ya ufadhili wa program ya Malala kwa wajumbe 64 wakiwemo walimu 40 na wakuu wa Shule 20 na maofisa elimu wanne kutoka wilaya nne za mkoa wa Tanga yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani humo.
Mmoja wa washiriki mwalimu wa shule ya sekondari Mwera ya wilaya ya Pangani, Teresia Kapinga akiwasilisha taarifa wakati wa mafunzo ya siku nne ya ujasiriamali yanayotolewa na UNESCO chini ya ufadhili wa program ya Malala kwa wajumbe 64 wakiwemo walimu 40 na wakuu wa Shule 20 na maofisa elimu wanne kutoka wilaya nne za mkoa wa Tanga yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani humo.
Pichani juu na chini ni washiriki wa mafunzo ya siku nne ya ujasiriamali yanayotolewa na UNESCO chini ya ufadhili wa program ya Malala kwa wajumbe 64 wakiwemo walimu 40 na wakuu wa Shule 20 na maofisa elimu wanne kutoka wilaya nne za mkoa wa Tanga yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani humo.


Mgeni rasmi Ofisa Elimu wa mkoa wa Tanga, Mayasa Hashimu (wan ne kushoto) katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya siku nne ya ujasiriamali yanayotolewa na UNESCO chini ya ufadhili wa program ya Malala kwa wajumbe 64 wakiwemo walimu 40 na wakuu wa Shule 20 na maofisa elimu wanne kutoka wilaya nne za mkoa wa Tanga yanayoendelea katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani humo.

No comments: