Na Emmanuel J. Shilatu
Kanali Mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Abdulrahman Omar Kinana anatajwa kuwa katika orodha ya safu za viongozi mibuyu na migude kwenye misitu minene ya siasa yenye kuhimili tufani za kila aina pia Mwanasiasa anayependa kuheshimu utamaduni, utaratibu na mwenye kuishi kwa misingi ya nidhamu .
Kinana anatajwa kama zao miongoni mwa kunga zitokanazo na mazao katika medani za siasa, utawala, uongozi na aliyeshiba ujuzi toshelezi wa masuala ya diplomasia ya siasa pia anayejua mahusiano yatokanayo na historia, harakati za ukombozi na umoja wa Afrika.
Sauti yake aghalabu huwa na mvumo wa mawimbi ya busara, fikara njema na hekima zenye wito pele aamuapo kusema, kukosoa, kutetea, kukumbusha, kushauri au kuonya kutokana na tabia yake ya kufanya yote hayo kwa hali ya kujiamini akiwa na nguvu ya hoja.
Ukimya wa Mwanasiasa huyo siku zote ni kama mfano wa Simba hodari awindae nyikani au mbugani akiwa hana pupa wala kiherehere. Huyafanya yote kwa utulivu na umakini mkubwa ambao baadae haumletei majuto, athari wala taathira.
Ni Mwanasiasa wa aina yake aliyewahi kuhitajiwa na Marais (Wenyeviti) watatu awe katibu mkuu wa CCM akakataa huku akitoa madai mazito yenye msingi, nguvu ya hoja na maana.
Amewahi kutakiwa na Rais Ali Hassan Mwinyi awe Katibu Mkuu wa CCM akakataa huku akitoa hoja. Akasema alikuwa na mchakato wa kazi nyeti na muhimu akishirikiana na wenzake kufanya mabadiliko ya mfumo mpya wa Jeshi utakaokwenda sanjari na mahitaji ya wakati; hivyo asingekuwa tayari kuiacha kabla kazi hiyo kukamilika.
Akatakiwa tena na Rais Benjamin Mkapa ashike nafasi hiyo akasita kukubali huku akitoa hoja za msingi na zenye mashiko yasio na shaka wala utata.
Kinana mara ya kwanza alitakiwa na Mwenyekiti Mstaafu Kikwete akakataa kubeba jukumu hilo kwa sababu kadhaa alizoona ni ngumu kwake kukitumikia chama kwa wakati huo. Hata hivyo mbinu za ushawishi zikafanyika akaafiki kuwa Katibu Mkuu.
Bila shaka Kinana aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wakati CCM ikiwa katika mgawanyiko mkubwa uliohatarisha uhai na mustakabali wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Kwa busara zake, pengine na ziada ya maarifa au mbinu za kijeshi, uzoefu wa kisiasa, uongozi na utawala, Chama Cha Mapinduzi na viongozi wake ghafla wakashikamana tena na kuzika yaliopita.
Amewahi kusema mbele ya Mzee Mkapa kwa wakati ule amejiona mbele yake bado ipo hazina ya Viongozi wajuzi wa muda mrefu ndani ya chama, vingunge wenye weledi na maarifa ya kisiasa kuliko yake hivyo muda wa yeye kushika wadhifa si wakati huo.
Akaachwa na kuendelea kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM akiwa Meneja wa kampeni za wagombea urais Mzee Mkapa na Dk. Jakaya Kikwete.
Katika safu ya Vijana wa TANU Youth League na baadae UVCCM waliolelewa kwenye mikono ya Wanasiasa kama kina Mwalimu Julius Nyerere, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, Sheikh Thabit Kombo Jecha, Mzee Rashid Kawawa, Mzee Saadan Abdul Kandoro na Mzee Rajab Diwani, Kinana anaweza kusimama kati yao.
Ameshiriki pamoja nao katika mbio za siasa, akichuma uzoefu huku mbele yake kukiwa na Wanasiasa kama Mzee Pius Msekwa, Marehemu Kingunge Ngombare Mwiru, Mzee John Malecela, Hayati Daudi Mwakawago, Hayati Moses Nnuye, Balozi Chrispher Liundi, Ali Ameir Mohamed na wengine kadhaa.
Vijana wanasiasia wa rika lake na wanaopishana kwa umri kiasi kidogo ni kina Dk Kikwete , Dk Mohamed Seif Khatib, Dk Salmin Amour, Yusuf Makamba, Jaka Mwambi, John Chiligati, Marehenu Ukiwaona Ditope Mzuzuri na wengine wengi .
Kanali Mstaafu Kinana kama atajigamba amezaliwa na kulelewa ndani ya TANU/ASP na maisha yake yote amekulia CCM na serikali zake, hoja hiyo itajuzu na kuyakinika.
Kwa ufupi ni Mwanasiasa asiyebahatisha katika utambuzi wa mizungu ya siasa, mbinu za utendaji, uelewa na upimaji kwenye viwango vya usemaji, ushauri au anapofanya shambulizi la kisiasa dhidi ya hasimu wake.
Niliposikia tetesi za kujiuzulu kwake kwa siku nzima ya jana nilikuwa nikitafakari bila kupata majibu ya haraka na kuona haikuwa wakati sahihi na muafaka sana kwa kiongozi huyo wa CCM kuachia ngazi na kujiweka kando.
Hata hivyo CCM ni chama kikongwe chenye hazina kubwa ya Wanasiasa hodari hivyo lolote linaweza kuwa ila muhimu ni kutega mingo na kusubiri wakati kwa kutega vyema masikio yetu.
*Shilatu E.J*
0767488622
No comments:
Post a Comment