ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 21, 2018

TPDC KUKIONGEZEA UZALISHAJI KIWANDA CHA DANGOTE-TANZANIA

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba (kutoka kulia waliokaa) akisani mkataba wa makubaliano na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha Saruji cha Dangote-Tanzania (wa kwanza) katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba (kutoka kulia) akibadilishana mkataba wa makubaliano na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha Saruji cha Dangote-Tanzania, Jagat Rathee (wa kwanza) katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba (katikati) akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam katika hafla fupi ya kusaini makubaliano na Kampuni ya Saruji ya Dangote-Tanzania ya kuwasambazia nishati ya gesi katika uzalishaji na kuachana na matumizi ya Dizeli katika uzalishaji wa umeme. Pembeni kulia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha Saruji cha Dangote-Tanzania na kushoni ni mmoja ya wafanyakazi wa TPDC.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha Saruji cha Dangote-Tanzania akizungumza na wanahabari katika hafla fupi ya kusaini makubaliano na Kampuni ya Saruji ya Dangote-Tanzania ya kuwasambazia nishati ya gesi katika uzalishaji na kuachana na matumizi ya Dizeli katika uzalishaji wa umeme. Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG. Katika kuunga mkono juhudi za serikali katika kampeni ya Tanzania ya Viwanda, Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesaini mkataba na Kampuni ya Saruji ya Dangote-Tanzania, utakaosaidia kiwanda hicho kuachana na matumizi ya mafuta ya dizeli katika uzalishaji wa umeme. Akizungumza jijini Dar es Salaaam wakati wa hafla fupi ya kusaini makubaliano hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba amesema mkataba huo na Dangote utadumu kwa miaka 20 tofauti na mikataba mingine ambao huingia na makampuni. "Tunajua Serikali iko kwenye hatua za kujenga uchumi wa viwanda, kwa hiyo sisi (TPDC) kwa nafasi yetu tutahakikisha viwanda vinazalisha bidhaa kwa gharama nafuu kupitia matumizi ya gesi, wataanza kutumia futi za ujazo milioni nane na baada ya miaka miwili ijayo wataanza kutumia futi za ujazo milioni 20,” amesema Mhandisi Musomba. Amesema kuwa tokea Septemba mwaka jana wao walikuwa tayari wameshafikisha huduma hiyo mlangoni mwa kiwanda cha Dangote, walichokuwa wanasubiri ni ukamilishwaji wa mitambo ili kuingiza gesi waanze matumizi. Kwa mujibu wa TPDC, kiwanda hicho ni sehemu ya viwanda saba vilivyopo kwenye mpango wa shirika katika mwaka wa fedha 2018/19, hivyo bado kuna vingine sita vitaunganishwa hapo baadaye. Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho cha Saruji, Jagat Rathee ameishukuru serikali kwa kuweza kuwawekeza nishati ya gesi ambao pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji lakini wataweza kutunza mazingira. "Kiwanda kilikuwa kinatumia wastani wa lita 106,000 za Dizeli ambazo zilizalisha wastani wa megawatt 20 (18MW -22MW) za gesi asilia kwa siku katika uzalishaji wa tani 2000 tu hivyo kutumia nishati ya gesi tutafikia wastani wa tani 6000 kwa siku huku gharama za uendeshaji zikishuka kwa asilimia 60. Kiwanda hicho kinaongeza idadi ya viwanda vinavyotumia gesi asilia kwa ajili ya uzalishaji wa umeme kufikia 42 nchini, ambavyo vinatumia futi za ujazo milioni 15 tu kutoka akiba ya futi za ujazo trilioni 57, zinazoweza kutumika miaka 40 ijayo nchini.

No comments: