Na Felix Mwagara, MOHA
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amelaani tukio lililofanywa na Mgambo wa Jiji la Dar es salaam akisema ni la kihuni, kishenzi na kinyama na halipaswi kufumbiwa macho na wapenda amani, watetezi wa haki za binadamu na wananchi wote kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Lugola alisema Serikali inalaani vikali tukio hilo ambalo lililotokea wiki iliyopita jijini humo, na kutokana na unyama huo tayari hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa.
“Jeshi la Polisi tayari limewakamata wahusika kama Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni tarehe 31 Agosti, 2018 ilivyoeleza. Natumia fursa hii kuwakumbusha tena Mgambo wote kuwa makini katika utekelezaji wa maagizo wanayopewa na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu,” alisema Lugola.
Pia kutokana na tukio hilo, Lugola alisema anazitaka Mamlaka za Majiji, Manispaa na Halmashauri kufikiria kuanzisha Huduma ya Polisi Wasaidizi (Auxiliary Police) katika maeneo yao kwa mujibu wa Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322 ili kuepuka matukio ya uvunjifu wa haki za Binadamu kama tukio la Mgambo watatu jinsi lilivyo tokea.
Aidha, Lugola pia alizungumzia kuhusu baadhi ya matukio mengine ambayo watu wanajichukulia Sheria mkononi na kuwaadhibu kwa kuwapiga watu wengine kwa sababu mbalimbali.
Aliyataja matukio hayo ni pamoja na ugomvi wa kifamilia ndani ya ndoa ambao huhusisha Wanaume kuwapiga wake zao au wake kuwapiga waume zao, pia wananchi kuwapiga watu wanaowatuhumu kwa makosa mbalimbali, pamoja na walimu kuwapiga wanafunzi kinyume cha sheria.
Pia Lugola aliwaonya baadhi ya Askari Polisi ambao wanatumia nguvu isiyo ya kadiri kulingana na mazingira halisi wanapowadhibiti watuhumiwa.
“Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Mambo ya Ndani ya Nchi inalaani vikali matukio ya kujichukulia Sheria mkononi na kupitia kwenu Wanahabari nawataka Watanzania kufuata sheria za nchi kwa kuacha vitendo vya kujichukulia Sheria mkononi. Vitendo hivi pamoja na kusababisha uvunjifu wa amani vinaweza kuleta madhara kwa watu ambao hawana makosa na kuichonganisha Serikali na wananchi wake,” alisema Lugola.
Kutokana na matukio hayo, Lugola aliwataka wanandoa wanakumbushwa kutumia Dawati la Jinsia katika Vituo vya Polisi kote nchini ili kuwasilisha malalamiko yao ya unyanyasaji wa kijinsia ndani ya ndoa ili hatua stahiki zichukuliwe.
Pia aliwataka wananchi waendelee kuheshimu sheria za nchi na kuepuka kujichukulia unakuta mtu anapigwa hata haulizi anayepigwa amekosa nini nae anajiunga nao na kumpiga hali ambayo imesababisha majeraha, vilema vya kudumu na vifo kwa watu wasio na hatia.
Hata hivyo, Lugola aliwaonya walimu kwa kufanya matukio kujirudia kwa kuwaadhibu wanafunzi kwa kuwachapa na kuwapiga hovyo kiasi cha kusababisha maumivu makali, ulemavu na vifo.
“Natumia fursa hii kuwakumbusha Walimu kote nchini kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ya Adhabu kwa wanafunzi ambayo imetolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuepuka madhara yake, kuondoa hofu kwa wazazi na kufanya shule zetu kuwa mahali salama kwa watoto wetu,” alisema Lugola.
No comments:
Post a Comment