ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 16, 2018

MAADHIMISHO YA SABA YA SIKU YA MARA (MARA DAY) YAFANYIKA NCHINI KENYA


Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya, Mhe. Simon Chelugui ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya saba ya Siku ya Mara akitoa hotuba ya ufunguzi ambayo ilielezea mikakati mbalimbali inayochukuliwa ili kukabiliana na vihatarishi vya kutokomeza ikolojia ya Mto Mara. 
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Mara yaliyofanyika kaunti ya Narok nchini Kenya




Maadhimisho ya Saba ya Siku ya Mara (Mara Day)

Bonde la mto Mara linalounganisha Tanzania na Kenya linashikilia uhai sio wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pekee, bali uhai wa nchi za Sudan, Ethiopia na Misri nazo kwa kiasi kikubwa unategemea bonde hilo.

Kauli hiyo ilitolewa na viongozi mbalimbali walioshiriki sherehe za maadhimisho ya saba ya Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika katika Kaunti ya Narok, Kenya siku ya Jumamosi tarehe 15 Septemba 2018. 

Maadhimisho ya Siku ya Mara ambayo kwa mwaka huu yalikuwa na kaulimbiu "Mto Mara unatuunganisha wote" hufanyika kwa kupokezana kati ya Tanzania na Kenya kila mwaka tarehe 15 Septemba kwa madhumuni ya kuhamasisha matumizi endelevu ya bonde la mto Mara.

“Siku ya Mara hailengi chochote, isipokuwa kutukumbusha jukumu letu la kutunza mazingira”, Gavana wa kaunti ya Narok, Mhe Samuel Oletunai alisema katika maadhimisho hayo.

Mhe. Samuel Oletunai aliwaasa Wakenya kutunza msitu wa Mau ambao ndio chanzo kikuu cha maji yanayotiririka mto Mara na kuiomba Serikali ya Kenya kuhakikisha kuwa mgogoro katika msitu huo unapatiwa ufumbuzi haraka. 

Mwakilishi wa Serikali ya Tanzania katika maadhimisho hayo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso (Mb) alieleza kuwa maji hayana mbadala kama chakula ambapo ukikosa wali utakula ugali, hivyo aliwahakikishia wadau waliohudhuria sherehe hizo kuwa Serikali ya Tanzania haitakuwa kikwazo cha harakati za kuhifadhi ikolojia ya mto Mara.

Utunzaji wa ikolojia ya mto huo ilielezwa kuwa ni muhimu kwa shughuli mbalimbali ikiwemo utalii na shughuli nyingine za kiuchumi ambapo Mwakilishi wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) katika sherehe hizo alisema kuwa Tanzania na Kenya zinapata zaidi ya Dola milioni 300 kwa mwaka kutokana na shughuli za kiuchumi katika mto Mara.

Tukio kubwa linalovutia watalii wengi duniani ni uhamaji wa wanyamapori aina ya nyumbu zaidi ya milioni 1.2 baina ya mbuga ya Serengeti nchini Tanzania na Masai Mara nchini Kenya katika kipindi cha Julai hadi Oktoba ambapo mara zote wanyama hao hukatiza mto Mara.

Mwakilishi huyo wa USAID alitaja sababu zinazoharibu ikolojia ya mto huo kuwa ni pamoja na uharibifu wa misitu, matumizi makubwa ya maji, ujenzi wa miundombinu mbalimbali na mmomonyoko wa udongo. Hivyo, aliahidi kuwa USAID itaendelea kushirikiana na wadau kukabiliana na changamoto hizo kwa kusaidia miradi ya maji na utunzaji wa mazingira. Alisema mto huo lazima uhifadhiwe kwa sababu ni mali ya watu waliopita, wasasa na wajao.

Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika sherehe hizo, Mhe. Simon Chelugui aliwahakikishia waliohudhuria maadhimisho hayo kuwa Serikali ya Kenya imejizatiti kulinda na kuhifadhi ikolokia ya mto Mara kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo. 

Hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Kenya, alizitaja kuwa ni pamoja na kuanzisha miradi ya maji na usafi katika mashule na aliutaja mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa na benki ya maendeleo ya Afrika kwenye mpaka wa Isebania ambao utawanufaisha pia Watanzania wanaoishi maeneo ya Sirari.

Sherehe hizo zilipambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo maonesho ya bidhaa na huduma ambao uzalishaji wake unazingatia uhifadhi wa mazingira.

Aidha, kulikuwa na burudani za ngoma, michezo ya mpira wa miguu mashairi, tunzo na ngojera ambazo zote zililenga kutoa ujumbe wa kuhimiza utunzaji wa mazingira. 
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. Pindi Chana akitoa salamu katika maadhimisho ya Siku ya Mara. 
Gavana wa akaunti ya Narok, Mhe. Samuel Oletunai akihutubia watu mbalimbali walioshiriki maadhimisho ya Siku ya Mara ambayo yalifanyika katika kaunti yake ya Narok.

Watu mbalimbali waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Mara wakifuatilia hotuba za viongozi. 
Mwakilishi wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) akivalishwa vazi la kimasai kabla hajatoa hotuba yake katika maadhimisho hayo. 
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Bibi Caroline Mthapula ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Adam Malima akitoa neno la mkoa katika maadhimisho hayo. 
Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dkt. Pindi Chana; Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Bibi Caroline Mthapula; Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso; Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya, Mhe. Simon Chelugui wakipata maelezo kutoka moja ya banda la maonesho ya Siku ya Mara kuhusu utunzaji wa mazingira. 
Mstari wa kulia kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dkt. Pindi Chana; Katibu Tawala wa mkoa wa Mara, Bibi Caroline Mthapula; Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso; Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya, Mhe. Simon Chelugui wakipata maelezo kutoka mmoja wa washiriki wa maonesho ya siku ya Mara namna anavyoshiriki katika shughuli za kutunza mazingira. 

No comments: