TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Maadhimisho ya Saba ya Siku ya Mara (Mara Day)
Bonde la mto Mara linalounganisha
Tanzania na Kenya linashikilia uhai sio wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
pekee, bali uhai wa nchi za Sudan, Ethiopia na Misri nazo kwa kiasi kikubwa
unategemea bonde hilo.
Kauli hiyo ilitolewa na viongozi
mbalimbali walioshiriki sherehe za maadhimisho ya saba ya Siku ya Mara (Mara
Day) zilizofanyika katika Kaunti ya Narok, Kenya siku ya Jumamosi tarehe 15
Septemba 2018.
Maadhimisho
ya Siku ya Mara ambayo kwa mwaka huu yalikuwa na kaulimbiu "Mto Mara
unatuunganisha wote" hufanyika kwa kupokezana kati ya Tanzania na Kenya
kila mwaka tarehe 15 Septemba kwa madhumuni ya kuhamasisha matumizi
endelevu ya bonde la mto Mara.
“Siku ya Mara hailengi chochote, isipokuwa
kutukumbusha jukumu letu la kutunza mazingira”, Gavana wa kaunti ya Narok, Mhe Samuel
Oletunai alisema katika maadhimisho hayo.
Mhe. Samuel Oletunai aliwaasa
Wakenya kutunza msitu wa Mau ambao ndio chanzo kikuu cha maji yanayotiririka
mto Mara na kuiomba Serikali ya Kenya kuhakikisha kuwa mgogoro katika msitu huo
unapatiwa ufumbuzi haraka.
Mwakilishi wa Serikali ya Tanzania
katika maadhimisho hayo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso
(Mb) alieleza kuwa maji hayana mbadala kama chakula ambapo ukikosa wali utakula
ugali, hivyo aliwahakikishia wadau waliohudhuria sherehe hizo kuwa Serikali ya
Tanzania haitakuwa kikwazo cha harakati za kuhifadhi ikolojia ya mto Mara.
Utunzaji wa ikolojia ya mto huo
ilielezwa kuwa ni muhimu kwa shughuli mbalimbali ikiwemo utalii na shughuli
nyingine za kiuchumi ambapo Mwakilishi wa Shirika la Misaada la Marekani
(USAID) katika sherehe hizo alisema kuwa Tanzania na Kenya zinapata zaidi ya
Dola milioni 300 kwa mwaka kutokana na shughuli
za kiuchumi katika mto Mara.
Tukio kubwa linalovutia watalii
wengi duniani ni uhamaji wa wanyamapori aina ya nyumbu zaidi ya milioni 1.2
baina ya mbuga ya Serengeti nchini Tanzania na Masai Mara nchini Kenya katika
kipindi cha Julai hadi Oktoba ambapo mara zote wanyama hao hukatiza mto Mara.
Mwakilishi huyo wa USAID alitaja
sababu zinazoharibu ikolojia ya mto huo kuwa ni pamoja na uharibifu wa misitu,
matumizi makubwa ya maji, ujenzi wa miundombinu mbalimbali na mmomonyoko wa
udongo. Hivyo, aliahidi kuwa USAID itaendelea kushirikiana na wadau kukabiliana
na changamoto hizo kwa kusaidia miradi ya maji na utunzaji wa mazingira.
Alisema mto huo lazima uhifadhiwe kwa sababu ni mali ya watu waliopita, wasasa
na wajao.
Waziri wa Maji na Usafi wa Kenya
ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika sherehe hizo, Mhe. Simon Chelugui
aliwahakikishia waliohudhuria maadhimisho hayo kuwa Serikali ya Kenya
imejizatiti kulinda na kuhifadhi ikolokia ya mto Mara kwa faida ya vizazi vya
sasa na vijavyo.
Hatua zinazochukuliwa na Serikali
ya Kenya, alizitaja kuwa ni pamoja na kuanzisha miradi ya maji na usafi katika
mashule na aliutaja mradi mkubwa wa maji unaofadhiliwa na benki ya maendeleo ya
Afrika kwenye mpaka wa Isebania ambao utawanufaisha pia Watanzania wanaoishi
maeneo ya Sirari.
Sherehe hizo zilipambwa na
shughuli mbalimbali zikiwemo maonesho ya bidhaa na huduma ambao uzalishaji wake
unazingatia uhifadhi wa mazingira.
Aidha, kulikuwa na burudani za
ngoma, michezo ya mpira wa miguu mashairi, tunzo na ngojera ambazo
zote zililenga kutoa ujumbe wa kuhimiza utunzaji wa mazingira.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,
Narok, kenya
16 Septemba 2018
|
No comments:
Post a Comment