ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 15, 2018

MAKAMU WA RAIS AZINDUA URITHI FESTIVAL

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kama ishara ya kuzindua rasmi Tamasha la Urithi (Urithi Festival) katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.  
 Mtoto wa Shaaban Robert, Mzee Ikbali Robert akionyesha Tuzo ya Nguli wa Lugha ya Kiswahili katika Uandishi ya Urithi Festival ya mwaka 2018 aliyokabidhiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ikiwa ishara ya kutambua mchango mkubwa wa Baba yake Mzee Shaaban Robert. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Tuzo ya Nguli wa Sanaa za Ngoma ya Urithi Festival mwaka 2018 Mjukuu wa Mzee Morris Nyunyusa kama ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika kutunza na kudumisha utamaduni. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia moja ya bidhaa zilizotengenezwa kwa mikono na kikundi cha Eddie Collection wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Urithi (Urithi Festival) kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kwa kutambua umuhimu wa sekta ya utalii kwa uchumi wa nchi yetu, na kwamba ili kuweza kupata watalii wengi zaidi lazima kuwa na usafiri wa anga ulio na uhakika; ndiyo maana Serikali imeamua kufufua shirika letu la ndege (ATCL) na tayari Serikali imenunua ndege mpya saba.

Makamu wa Rais ameyasema hayo leo wakati wa sherehe za uzinduzi wa Tamasha la Mwezi  wa Urithi wa Utamaduni wa Mtanzania linalojulikana kama Urithi Festival liliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma.

“Ni wazi pia kwamba utalii unahitaji usafiri bora na wa uhakika wa nchi kavu, hususan reli na barabara.  Kwa kujua hili, Serikali imeamua kujenga reli mpya ya Standard Gauge kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, katika awamu hii ya kwanza. Vilevile, Serikali inakarabati reli yetu ya zamani kutoka Tanga hadi Arusha. Ukarabati wa reli hii utawezesha pia kuanzisha utalii wa reli (railway tourism) utakaohusisha vivutio mbalimbali, hususan Milima ya Usambara (Lushoto), Hifadhi ya Taifa Mkomazi, na Mlima Kilimanjaro. Kwa upande wa barabara, barabara nyingi kuu na za mijini zinajengwa kwa kiwango cha lami.” Alisema Makamu wa Rais

Makamu wa Rais amebainisha kuwa Tanzania ni nchi iliyojaliwa kuwa na rasilimali nyingi za asili ikiwemo milima, misitu, mito, maziwa, bahari, wanyama wa aina mbalimbali na urithi wa utamaduni wa aina mbalimbali.

Makamu wa Rais amesisitiza ni vyema kwa umoja wetu tuweke nguvu kufanya Urithi wa utamaduni wetu kuwa ni zao la uhakika kwenye sekta ya utalii na ukarimu. Vilevile, thamani ya utamaduni inaonekana kwenye sekta nyingine kama elimu, afya, michezo, kilimo, viwanda na maendeleo ya jamii.

 Katika Tamasha hilo ambalo lilitanguliwa na burudani mbali mbali za ngoma na nyimbo za asili pia Viongozi wa Serikali na Taasisi mbali mbali walihudhuria.

Aidha Wasanii Nguli katika lugha ya kiswahili, sanaa na utamaduni walitunukiwa Tuzo, wasanii hao ni Shaaban Robert ambaye alitunukiwa Tuzo ya Nguli wa Lugha ya Kiswahili katika Uandishi ya Urithi Festival mwaka 2018 na kupokelewa na Mtoto wake Ikbali Robert, na Mzee Morris Nyunyusa ambaye alitunukiwa Tuzo ya Nguli wa Sanaa za Ngoma ya Urithi Festival kwa mwaka 2018 ambayo ilipokelewa na mjukuu wake.

No comments: