Serikali imesema itaanza kuandika sheria zote pamoja miswada na inayowasilishwa bungeni kwa lugha ya Kiswahili.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Jumatano Septemba 5, wakati akitoa ufafanuzi kuhusu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Faida Bakari aliyetaka mahakama ziendeshe kesi na kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili sanjari na miswada na sheria mbalimbali zinazowasilishwa bungeni.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Rais wetu anakienzi Kiswahili na lugha hiyo ndiyo lugha yetu rasmi, lakini miswada inayowasilishwa hapa inawasilishwa kwa Kiingereza si wote tunafahamu lughha hiyo, je serikali haion i umuhimu wa kutumia lugha hiyo,” amehoji.
Akitoa ufafanuzi wa kisheria, Dk. Kilangi amesema nafasi ipo kwamba mashtaka kama mashtaka yanaendeshwa kwa Hakimu au Jaji anaweza kuruhusu yaendelee kwa Kiswahili au Kiingereza.
“Lakini kuhusu miswada na sheria kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili, hilo liko katika mpango wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuanza na kutafsiri karibu sheria zote ziwe na zisomeke kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu ndiyo lugha inayozungumzwa na kueleweka na watu wote.
“Lakini suala hili linahitaji rasilimali na tuna changamoto kidogo za rasilimali na wataalamu wa kutosha kwa sababu kuna hatari maana sheria ina lugha yake ukitafsiri tu moja kwa moja kwenda Kiswahili kuna changamoto pia ya kupoteza mantiki iliyokusudiwa.
“Kwa hiyo tuna changamoto pia ya kuwa na wataalamu wanaoweza kutufanyia kazi hii kwa usahihi walau ni kati ya mambo ambayo tumeyawekea mipango tuanze kuyafanyia kazi kwamba sheria zote ziandikwe kwa lugha ya Kiswahili,” amsema Dk. Kilangi.
No comments:
Post a Comment