Waziri Ummy alitoa kauli akiwa Dodoma wakati akizindua maadhimisho ya siku ya tiba asili ya Mwafrika, ambayo iliadhimishwa wiki iliyopita katika kliniki ya mganga wa tiba asili ya Golden Sanitarium iliyopo jijini hapo.
Amesema katika kurasimisha huduma za tiba asili nchini, waganga wa tiba asili ni lazima waboreshe huduma zao kwa kusajiliwa wao wenyewe na kuwaorodhesha wasaidizi wao, kusajili vituo vyao vilivyoboreshwa na kusajili dawa za asili zilizotengenezwa viwandani.
Kwa agizo hilo, tunaomba kuwasisitiza waganga wa jadi kwamba mbali na kutoa huduma ya tiba, lakini ni wajibu wao kuhakikisha mazingira wanakofanyia kazi yanakuwa rafiki kwa wagonjwa ndio maana kokote mahali kulipo na hospitali ni kusafi duniani kote.
Kazi zinazofanywa na waganga wa jadi haziko mbali sana na zile zinazofanyika hospitalini iwe za binafsi au za umma, mazingira yake ni lazima yawe katika hali ya usafi. Si hivyo tu, pia dunia inabadilika kila kukicha hasa katika teknolojia.
Tunaamini ni muda mwafaka waganga wa jadi kubuni njia za kisasa, ikiwamo ya kutunza kumbukumbu ya tiba yao kwa njia ya kompyuta kwani hii itawasaidia kuwa na marejeo hata kwa wengine ambao kwa kutumia mitandao, wanaweza kubadilishana uzoefu.
Tunaamini ni wakati sasa, kama Waziri Ummy alivyoagiza, waganga wa jadi kubadilisha njia zao za zamani na kwenda na kisasa ambapo dunia imekuwa kijiji kwani wanaweza kutumia mitandao kujifunza jinsi ya kuhudumia wagonjwa wa aina fulani kwa kutumia dawa ambazo asili yake ni nchi nyingine ilimradi wajiweke katika mitandao iliyopo hivi sasa duniani.
Mbali na hayo, Waziri Ummy pia akawataka waganga kuhakikisha wanatoa huduma zako kwa kuzingatia maadili ya taaluma na kumjali mteja.
Maadili ya kazi yanaendana na taaluma, hivyo tunaamini waganga popote wanapofanya kazi, kutimiza maagizo haya ili kuifanya kazi hii iheshimike kwani wao wana umuhimu mkubwa katika jamii kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
Ni kutokana na ukweli huu, Waziri Ummy akasema hata serikali itaendelea kuhakikisha kuwa tiba asili inaboreshwa na kuendelezwa na kwa kufanya hivyo, kutasaidia kuwahudumia watanzania wengi na pia itaondoa migongano katika jamii ya kuhusisha tiba asili na ushirikia na uchawi.
Akasema kuanzia sasa vituo vya afya vya serikali vitaanza kutoa mafunzo kwa waganga wa tiba asili ili kupata uelewa wa kuwahudumia wananchi na kuwataka waganga hao kutumia fursa hiyo kwa kuhudhuria kikamilifu.
Hata hivyo ili haya yaweze kutimia, Waziri Ummy akawataka waganga na wadau wa tiba asili kuzingatia sera, sheria, kanuni, miongozo na taratibu zinazowasimamia katika kutoa huduma za tiba asili kwa wateja wao na kukemea utoaji wa matangazo yanayokinzana na sheria.
Tunaamini, waganga wa jadi watafanya kama walivyoelekezwa ili kuwezesha jamii kundelea kuwaamini huku serikali ikiendelea kuwapa kila msaada ili wanaohitaji huduma waweze kunufaika.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment