Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi akikagua jengo la kituo kipya cha Polisi ambacho kilijengwa toka mwaka 2010 lakini bado hakijamalizika, kushoto kwake ni Mkuu wa Polisi wilaya ya Longido Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Joswam Israel Kaijanante.
Jengo la kituo kipya cha Polisi Kamwanga ambacho kimejengwa kwa nguvu ya wananchi toka mwaka 2010 ambacho kikikamilika kitaongeza idadi ya askari ambao watahudumia katika eneo hilo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi akiongea na wananchi wa kata ya Kamwanga wilayani Longido mara baada ya kufanya harambee ya kuwezesha umaliziaji wa ujenzi wa kituo hicho. (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha)
Chifu wa eneo la Endonet Count ya Kajiado nchini Kenya Bw. Jacob Lemunge akiongea na wananchi waliohudhuria katika shughuli ya harambee ya kuchangia umaliziaji wa ujenzi wa kituo kipya cha Polisi Kamwanga kabla ya kuongoza wananchi wa Kenya kuchangia, pembeni yake ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha (SACP) Ramadhani Ng'anzi. (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha)
Na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha
Katika hali ya kujenga mahusiano ya nchi jirani pamoja na kutoa kipaumbele kwa suala zima la ulinzi na usalama bila kujali utaifa, Chifu wa eneo la Endonet, Count ya Kajiado ya nchini Kenya Bw. Jacob Lemunge aliwaongoza baadhi ya wananchi wa Kenya kuchangia ujenzi wa kituo kipya cha Polisi cha Kamwanga kilichopo wilaya ya Longido.
Chifu Lemunge aliwaongoza wananchi wa Kenya ambao wanaishi mpakani mwa eneo hilo, kuchangia kituo hicho kipya wakati wa harambee iliyoongozwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi
Chief Lemunge alisema kwamba wameamua kufanya hivyo kwa kuwa suala la usalama ni muhimu kwa pande zote huku ikizingatiwa kwamba jamii zote za Wakenya na Watanzania zinaishi mpakani na kunapotokea tatizo la kiusalama upande mmoja, basi wanaoathirika ni wote.
Akizungumza mara baada ya harambee hiyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi licha ya kuwashukuru wananchi wa Kamwanga na majirani zao upande wa Kenya kwa kushikamana, alisema kwamba kitu cha kwanza katika maisha ya binadamu ni ulinzi.
Alisema bila kuwepo kwa usalama katika eneo lolote hakuna shughuli zozote za maendeleo zitakazofanyika na kuongeza kwamba hata eneo hilo linahitaji uimarishaji wa ulinzi kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
“Eneo lolote linapopiga hatua kiuchumi na kama hakuna ulinzi wa kutosha basi litakuwa linashawishi kuwepo au kuongezeka kwa uhalifu, hivyo nami sitataka kusikia eneo hili ambayo ni himaya yangu linatawaliwa na wahalifu”. Alifafanua Kamanda Ng’anzi.
Kamanda Ng’anzi aliahidi kukipandisha daraja kituo hicho kutoka daraja” C” mpaka kufikia daraja “B” sambamba na kuongeza idadi ya askari pindi tu kitakapokamilika.
Kwa upande wa mhamasishaji wa ujenzi wa kituo cha awali ambacho kinatumika mpaka hivi sasa Mzee Hendry Daniel maarufu kwa jina la Sawaki alisema kwamba mwaka 1998 aliamua kuhamasisha wananchi wa eneo hilo kujenga kituo kwa kuwa kulikuwa na matukio ya kijinai yaliyokuwa yanatokea lakini hapakuwa na sehemu ya kushtaki.
“Tulikuwa tunapata tabu sana na tulikuwa tunaishi kama wanyama yaani ukifanyiwa kosa hakuna hata sehemu ya kushtaki labda uende Tarakea ambapo ni mbali zaidi kutoka hapa”. Alisema Mzee Sawaki.
Harambee ya ujenzi wa kituo hicho kipya ambacho kilianza kujengwa mwaka 2010 ililenga kupata fedha kwa ajili ya umaliziaji, ambapo wananchi wa kutoka maeneo mbalimbali ya Tarafa ya Enduimeti walijitolea kutoa fedha taslimu huku wengine wakitoa ahadi ya fedha na vifaa.
No comments:
Post a Comment