Advertisements

Friday, October 19, 2018

SERA YA DIPLOMASIA YA UCHUMI INAVYOLETA MAGEUZI YA UWEKEZAJI

Na. Immaculate Makilika
MAELEZO
DAR ES SALAAM
18.10.2018

KATIKA miaka ya 1960 hadi 1980 malengo ya ziada katika Sera ya mambo ya nje ya Tanzania yalikuwa ni ukombozi wa Bara la Afrika kutoka kwa makucha ya ukoloni na ubaguzi wa rangi.

Baada ya kukamilisha juhudi hizo, Tanzania ilifanya mageuzi makubwa katika Sera ya Mambo ya Nje iliyoweka msisitizo wa diplomasia ya uchumi ili kusukuma maendeleo ya Taifa.

Diplomasia ya uchumi ni msisitizo wa Sera ya Mambo ya Nje yenye mikakati, malengo, mbinu na maarifa yanayoelekeza taifa kupata na kuvuna rasilimali na utaalam kutoka jumuiya ya mataifa ili kuleta na kuchochea maendeleo ya taifa husika.

Mwaka 2001 Tanzania ilipitisha sera hiyo ili kuharakisha maendeleo hasa katika mageuzi ya kiuchumi kupitia uwekezaji, ambapo katika mwendelezo huo Serikali ya Awamu hii ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeongeza kasi ya utekelezaji wa sera ili kuifanya Tanzania kufikia nchi ya kipato cha uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Azma hii inamaanisha kuwa diplomasia ya uchumi lazima iongeze mkakati wa Diplomasia wa viwanda ili kutekeleza maono na mawazo ya Rais Dkt. Dkt. John Pombe Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kupitia malighafi za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masahriki kwa mwaka 2018/2019, Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga anasema kuwa sera ya diplomasia ya uchumi imeweka vipaumbele katika uwekezaji, miundombinu ikiwa ni pamoja na nishati, biashara na masoko ya bidhaa kutoka viwandani, kilimo, utalii na madini

Aidha, Balozi Mahiga anasema kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025, ambapo hivi karibuni Wizara hiyo imeratibu maonesho ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya Tanzania, yaliyofanyika mjini Nairobi nchini Kenya.

“Katika maonesho hayo ya kipekee kuwahi kufanywa na Tanzania huko nchini Kenya jumla ya kampuni 27 zinazozalisha bidhaa za viwandani kutoka Tanzania zilishiriki ili kutangaza bidhaa na kuvutia utalii, ambapo yaliyotoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kutafuta masoko nchini humo na kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili” anasema Waziri Mahiga.

Aidha, Balozi Mahiga anasema kupitia sera ya diplomasia ya uchumi, Serikali za Tanzania na Misri, zimeratibu majadiliano ya pamoja hatua iliyosaidia kuondoleana ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 100, huku Tanzania ikiondoa ushuru kwa kiwango cha asilimia 96.89, ambapo kiwango kilichosalia kitaondolewa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katika kuchagiza sera hiyo, Dkt. Mahiga anasema mwezi Februari, mwaka huu, Serikali za Tanzania na Korea Kusini ziliandaa kongamano la biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili, kufuatia mazungumzo baina ya viongozi wa kampuni ya Hyundai na Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC).

Aidha, Balozi Mahiga anasema aliwataka wadau wanaosimamia masuala ya biashara na uwekezaji kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji wanaoonesha nia ya kuwekeza nchini.

MWISHO

No comments: