Iringa. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwele amewataka watendaji wa wizara yake kuongeza bidii ya kazi ili kumuepusha na fagio lililowakuta aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage.
“Maana mmesikia Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) akishatumwa na Mheshimiwa Rais (John Magufuli) kwako, maana yake kuna kitu umeshindwa kufanya. Tusiruhusu hilo likafika, vinginevyo nitang’oka,” alisema.
Dk Tizeba na Mwijage walitupwa nje ya Baraza la Mawaziri huku Rais Magufuli akibainisha kwamba walishindwa kutimiza vyema majukumu yao katika kushughulikia changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza katika wizara zao likiwamo sakata la bei ya korosho kiasi cha kulazimika kumtuma Waziri Mkuu.
Nafasi za mawaziri hao zilijazwa na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga aliyeteuliwa na RaisMagufuli kuwa Waziri wa Kilimo na Joseph Kakunda, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Akifungua mkutano wa siku mbili wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), mjini Iringa jana, Kamwele alisema; “Nitajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili Waziri Mkuu asitumwe wizarani kwangu kama ilivyotokea katika wizara zingine.”
Akitoa maagizo mbalimbali kwa watendaji hao wa Tanroads, Kamwele aliwataka watatue kero za wananchi pasipo kusubiri matamko kutoka kwa watendaji au viongozi wa ngazi za juu.
Alisema yapo mambo mengi yanayoweza kufanywa na watendaji wa chini lakini yamekuwa yakikwama kwa sababu ya kufanya kazi kwa mazoea kunakosubiri matamko ya viongozi, au ziara ya naibu waziri, waziri, waziri mkuu au Rais mwenyewe.
“Mie nina tatizo bandarini Dar es Salaam, mizigo inayopitia pale ni mingi lakini tuna mabehewa 355 tu. Nimekutana na Rais na nimemueleza mahitaji yetu ni mabehewa mengine 800,” alisema.
Waziri huyo alisema changamoto hiyo ni kubwa na kama angeendelea kukaa nayo kimya, huenda Rais angemtuma Waziri Mkuu na matokeo yake angeonekana ana upungufu na isingeshangaza kama angechukuliwa hatua.
Alisema changamoto nyingine wizarani kwake ni ucheleweshaji wa makadiro ya kodi ya mizigo inayopitia katika bandari hiyo. Alisema ufanisi wa bandari hiyo inayopokea meli zaidi ya 1,000 kila mwezi, unaonekana mdogo kwa sababu ya mrundikano wa mizigo.
Alisema akitoka Iringa atakwenda Dodoma kukutana na Waziri wa Fedha kujua namna ya kushughulikia tatizo hilo kwa haraka.
“Nini kinakwamisha makadiro hayo kufanywa kwa muda mfupi ili kuondoa mrundikano huo, kwa nini ichukue siku 20 hadi zaidi ya 30,” alisema.
Alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imepanga kuanza na kukamilisha miradi mbalimbali ya barabara, kujenga reli ya kisasa, meli na vivuko kwenye Ziwa Victoria na kununua ndege nne ili kuimarisha huduma ya usafiri, “Mipango hii ni mikubwa ambayo utekelezaji wake unahitaji utendaji mzuri kutoka kwenu na kwa kutanguliza uzalendo.”
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi alimkumbusha waziri huyo ahadi ya ujenzi wa barabara ya Iringa hadi Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa kiwango cha lami akisema mpango huo ni muhimu katika mikakati ya mkoa ya kukuza utalii kwa mikoa ya Kusini mwa Tanzania.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Patrick Mfugale ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Tanroads, alizungumzia mikakati mipya ya ujenzi wa barabara za lami nchini, akisema ujenzi utazingatia mazingira ya eneo husika.
No comments:
Post a Comment