ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 23, 2018

SERIKALI KUWASHUGHULIKIA WANANCHI WANAOHARIBU MIUNDOMBINU YA NJIA YA RELI

 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akisikiliza kwa makini taarifa kuhusu mataruma yanayohitajika kukarabati njia ya reli ya Korogwe – Mombo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Reli wa Shirika la Reli Tanzania Mhandisi Felix Nlalio (wa kwanza kushoto) akiwa kwenye ziara ya kukagua reli hiyo mkoani Tanga. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Gwakisa Kasongwa
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (mwenye kikoti cha njano) akipata maelezo kuhusu vifungashio vya mataruma ya reli vinavyohitajika kwa ajili ya kukarabati njia ya reli ya Dar es Salaam – Moshi kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Reli wa Shirika la Reli Tanzania Mhandisi Felix Nlalio (aliyeinama) wakati wa ziara yake mkoani Tanga ya kukagua ukarabati wa reli hiyo.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akipanda  kiberenge kwa ajili ya ziara ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya njia ya reli ya Dar es Salaam – Moshi katika stesheni ya Mombo mkoani Tanga

Serikali inawataadharisha wananchi wanaoharibu miundombinu ya njia ya reli kwa kuwa imeazimia kuwachukulia hatua kwa wanaojishughulisha na shughuli za kibinadamu ndani ya eneo la hifadhi ya miundombinu ya njia ya reli na kwa wanohujumu miundombinu hiyo kwa kuiba 
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake ya kukagua ukarabati wa miundombinu ya njia ya reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Arusha akiwa kwenye stesheni ya treni ya Mombo iliyopo mkoani Tanga 
Nditiye ameyasema hayo kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Gwakisa Kasongwa akiwa na kamati yake ya ulinzi na usalama kuwa washirikiane na Shirika la Reli Tanzania (TRC), viongozi na wananchi wanaoishi maeneo inakopita reli hiyo na vyombo vya ulinzi na usalama kuilinda na kuitunza reli kwa kuwa reli ni uchumi na inachangia maendeleo ya taifa letu, tuilinde na tuitunze. “Ni marufuku kufanya shughuli yoyote ya kibanadamu ndani ya eneo la mita 30 kulia na kushoto mwa njia ya reli kwa kuwa kwa kufanya shughuli za kilimo au kibinadamu unasababisha udongo kuja kwenye njia ya reli na kuharibu miundombinu ya njia ya reli,” amesema Nditiye.
Pia ameongeza kuwa wapo baadhi ya wananchi wanahujumu reli yetu, wanafungua vifungashio ambapo inaweza kusababisha treni kuanguka kwa lengo la kutaka kuiba mataruma na reli yenyewe, viwanda vya chuma chakavu wafikie mahala watafute malighafi inayotakiwa.  Amesema kuwa treni ikirushiwa mawe wakati inatembea na ikitokea kioo kikapasuka, treni hiyo isimame na wananchi waishio eneo hilo wachukuliwe hatua
Nditiye amesema kuwa hakuna Serikali makini inaweza kupuuza usafiri wa njia ya reli ambapo kwa kutambua hilo, Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Serikali ya Awamu ya Tano ameona afufue reli hii ambayo inatakiwa ianze kufanya kazi ifikapo mwishoni mwa mwaka 2018. Amefafanua kuwa reli ni usafiri wa gharama nafuu na starehe na itasaidia kuzuia uharibifu wa barabara kwa kusafirisha mizigo mizito
Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Gwakisa Kasongwa amesema kuwa watashirikiana na TRC kuhakikisha kuwa wanalinda rasilimali za reli, “reli ni rasilimali zetu,” amesema Kasongwa. Vile vile, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Korogwe kusimamia, kufuatilia na kuwadhibiti na kuwachukulia hatua wananchi wanaolima karibu na miundombinu ya reli ili udongo usiathiri reli hiyo. Pia, ameomba ukarabati wa reli hiyo ukamilike kwa kuwa reli ni fursa kubwa kwa wananchi wa Korogwe. “Reli hii ni fursa kubwa kwa wana Korogwe, tunaomba reli ikamilike ili kuinua uchumi wa wananchi wa Korogwe”, amesisitiza Kasongwa. 
Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Reli wa TRC Mhandisi Felix Nlalio amemweleza Nditiye kuwa kazi ya kufufua reli hiyo ilianza mwezi Oktoba, 2017 kwa kukarabati njia ya reli na madaraja kutoka Korogwe hadi Mombo ambapo ukarabati umekamilika kwa asilimia 100 na umegharimu kiasia cha shilingi milioni 627 kwa kurudisha reli, mataruma na vifungashio vilivyokuwa vimeibiwa, kubadilisha mataruma ya mbao kwenye madaraja makubwa, kujenga makaravati, kuondoa udongo uliokuwa umefunika miundombinu ya reli na kufyeka majani na vichaka. 
 Amefafanua kuwa kazi ya ukarabati ya miundombinu ya njia ya reli inaendelea kati ya stesheni ya Momo na Same ambao umeanza mwezi Novemba, 2018 ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ambao unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.03 ambapo utahusisha ukarabati wa miundombinu ya njia ya reli hiyo kwa kuwa sehemu hiyo ilipata uharibifu mkubwa kwa kuoshwa na mafuriko ambapo una mahitaji makubwa ya ujenzi wa miundombinu ya maji ikiwemo madaraja ya kati na madogo, ujenzi wa nguzo za madaraja, utandikaji upya wa reli kipande cha kilomita 6.5, kurudishia vifungashio vya mataruma 62,000 vilivyoibiwa, kurudishia vifungashio vya reli  - chuma mbili pea 3,000 zilizoibiwa na kukarabati majengo.
Amesema kuwa hadi sasa ukarabati huo umeiwezesha njia ya reli kupitika vizuri. Nlalio amefafanua kuwa wananchi wameiba vifungashio vya reli vipatavyo pea 3,000 na vifungashio vya mataruma 62,000 ambavyo vinahitajika kurudishiwa ambapo ametoa rai kwa wananchi kuilinda na kuitunza reli yetu kwa kuwa reli nayo ni mwananchi anayeishi maeneo yao
Ziara hiyo imeratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu Tanzania (SUMATRA) kwa lengo la kuhakikisha kuwa miundombinu ya nchi kavu ncini ikwemo miundombinu ya reli inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyombo vya usafiri vya taasisi za Serikali na za sekta binafsi. 

No comments: