ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 10, 2018

MAHAKAMA YAELEZWA MKURUGENZI KAMPUNI YA KILUWA STEAL GROUP CO.LTD ALIVYOPATA HATI ZA VIWANJA 70 KIHALALI

*Shahidi asema Kiluwa alipata viwanja hivyo kwa utaratibu wa kawaida
*Akana kuomba wala kupokea rushwa...aeleza namna hati zilivyomfikia

Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam imeelezwa kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Steal Group. Co.ltd na Kiluwa Free Processing Zone, Mohamed Kiluwa (50)  alipata hati za viwanja 70 
kihalali kwa kufuata taratibu zote za ardhi.

 Kamishna Msaidizi wa Ardhi, Mathew Nhonge ambaye ni shahidi wanne wa upande wa mashtaka, ameyasema hayo leo  mbele ya Hakimu Mkazi Samweli Obas, alipokuwa akitoa ushahidi dhidi ya kesi ya kutoa rushwa Sh.milioni 90 kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi

Akijibu maswali ya Wakili wa utetezi Imani Madega, shahidi huyo amedai Kilua alipata viwanja hivyo kutoka Halmashauri kwa utaratibu wa kawaida na viwanja hivyo vyote vilipimwa na ardhi.

Anadai hati zote zilizosainiwa kila kitu katika hati hizo kilikuwa sawa sawa na aliridhika nazo ndio sababu alisaini. Alipohojiwa kama katika mchakato wote huo walimuomba fedha mshtakiwa au alipewa fedha yoyote, shahidi alikana kuwa hajapewa fedha wala kuomba hela kwa Kilua. Pia amedai hakuona wakati rushwa hiyo ikitolewa, hati za mshtakiwa alizipata kihalali na endapo Mahakama itaamua vinginevyo Wizara haitabisha .

Wakati akitoa ushahidi wake, shahidi huyo akiongozwa  na Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo, shahidi Mathew amedai Kampuni ya Kilua iliomba kumiliki ardhi maeneo ya Kikongo wilayani Kibaha, hati za kumiliki 
viwanja 73 zilimfikia kwa ajili ya kuzisaini. 


Amedai katika hati hizo, hati 70  zilisainiwa kisha kupelekwa kwa Msajili wa hati na hati tatu hazikusainiwa kwa sababu zilikuwa na mapungufu.Shahidi huyo amedai, baada ya kusainiwa kwa hati hizo, Julai 13 mwaka huu alipigiwa simu na Waziri Lukuvi akimuelekeza amfahamishe Kilua aende ofisini kwake akiwa na hati zake. 

Pia amedai alimpigia mtu aliyemtaja kwa jina la Shabani na kumtaka amfikishie taarifa Kilua ambapo Julai 16 mwaka huu, Kilua alienda 
ofisini kwa Waziri aliyetaka hati hizo ziongezewe masharti kudhibiti hasa katika uwekezaji wa viwanda. Mathew ameendelea kudai, Kilua alifika kwa Waziri baada ya kukutana naye mapokezi ya kwenda ofisini kwa Waziri lakini amedai hakujua kilichondelea mpaka aliposikia kwa watumishi wa wizara kwamba Kilua kakamatwa kwa rushwa. 

Amedai, kutokana na kuwepo kwa taarufa hizo za suala la rushwa hati zote 70 zilifutwa katika usajili chini ya kifungu namba 178 cha sheria ya ardhi namba nne,"alidai. Katika kesi hiyo, inadaiwa Julai 16, mwaka huu kati ya saa sita na saa nane mchana akiwa Mkurugenzi wa kampuni hizo mbili alitoa rushwa ya Dola za Marekani 40,000 ambazo ni sawa na Sh.milioni 90 kwa Waziri Lukuvi.

Mshtakiwa anadaiwa kutoa fedha hizo kwa lengo la kwamba asiwasilishe hati ya umiliki wa kiwanja namba 57 Block B Kikongo na D Disunyura kilichopo eneo la viwanda lililopo Kibaha mkoani Pwani.

No comments: