ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 20, 2018

Rukwa wapokea vifaa vya Shilingi Milioni 211 kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto

Wakuu wa Wilaya za Sumbawanga, Kalambo na NKasi (kushoto) wakiweka saini mkataba wa usimamizi wa huduma za afya ya uzazi na mtoto mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) katika hafla fupi ya uzinduzi wa Kampeni ya “JIONGEZE TUWAVUSHE SALAMA” katika Mkoa wa Rukwa.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ( wa pili toka kulia) akipewa maelezo ya kitaalamu juu ya matumizi ya vifaa tiba vilivyotolewa na mradi wa Uzazi Salama na mmoja wa wawakilishi wa mradi huo (wa kwanza Kulia).
Baadhi ya Vifaa tiba vilivyotolewa na mradi wa Uzazi salama Mkoa wa Rukwa kwa Ofsi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Mradi wa uzazi salama Mkoani Rukwa umekabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi 211,145,850/= kwa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa ili kuvisambaza katika vituo 198 vya kutolea huduma za afya, ikiwa ni muendelezo wa jitihada na dhamira yao  ya kuhakikisha wanashirikiana na Mkoa katika kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto katika Mkoa.

Mradi huo unaoundwa kwa ushirikiano wa mashirika matatu ya Plan International Tanzania, AFRICARE na JHPIEGO kwa ufadhili wa serikali ya watu wa Canada umekabidhi vifaa hivyo vikiwemo vitanda vya kujifungulia, vifaa vya upasuaji kwa kinamama wajawazito, vifaa vya kumsaidia mtoto mchanga na mama kupumua, vifaa vya kuwasaidia watoto njiti, majokofu ya kuhifadhia damu na vifaa vya kufanyia tathmini ya hali ya lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanaratibu kufanyika kwa siku ya afya kwa mwaka mara moja kwa kila kijiji na kuwataka wakuu wa wilaya wasimamie zoezi hilo. Na kuwaomba wanaume, wazee na viongozi wote wa dini pamoja na vijiji kutambua jukumu la afya ya uzazi na mtoto pamoja na familia ni la wote na sio la kinamama na wanawake peke yao.

“Viongozi wa serikali katika ngazi za vijiji na kata wanao wajibu wa kuhakikisha akina mama wanahudhuria katika vituo vya afya pindi wanapojigundua ni wajawazito kwa huduma na ushauri wa kiafya. Tuwe mstari wa mbele kuelimisha wengine hasa vijana wetu kuhusu afya ya uzazi na kuwasisitiza kushiriki katika matukio mbalimbali yahusuyo afya kama huduma rafiki kwa vijana na siku ya afya ya kijiji “village health day” yanayoratibiwa na mradi wa Uzazi Salama.”

Nae Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Plan International Tanzania Paul Lusato aliziomba halmashauri pamoja na vituo vinavyotoa huduma za afya vitakavyopatiwa vifaa hivyo kuhakikisha wanavitunza vizuri ili kuendelea kutoa huduma tarajiwa kwa wananchi.

“Tunashauri pia viongozi katika ngazi ya mkoa kuendelea kutembelea maeneo ambayo wadau mbalimbali wa maendeleo wametoa msaada ili kujiridhisha kuwa uwekezaji uliofanywa unathaminiwa na kutunzwa na kuwa na manufaa yaliyotarajiwa,” Alibainisha.

Awali akitoa taarifa ya huduma za afya ya uzazi na mtoto Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alieleza kuwa katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka 2018 tayari kina mama 39 wameshapoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi ambayo ni sawa na uwiano wa vifo 97 kati ya vizazi hai 100,000 huku watoto wachanga 537 wakipoteza maisha kwa kipindi hicho hicho ambao ni sawa na uwiano wa vifo 14 katika kila vizazi hai 1000.


Makabidhiano hayo yamefanyika pamoja na uzinduzi wa kampeni inayojulikana kwa jina la “JIONGEZE TUWAVUSHE SALAMA” katika Mkoa wa Rukwa, Kampeni ambayo ilizinduliwa kitaifa tarehe 6 Novemba, 2018 na Mh.Samia Suluhu Hassani, Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayolenga kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga nchini Tanzania.

No comments: