Mkurugezi wa Huduma za Uuguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Sista Zuhura Mawona akipokea msaada wa mshine ya kusaidia wagonjwa wenye matatizo kwenye mfumo wa hewa kutoka kwa Elizabeth Amandus baada ya mtoto wake kupatiwa huduma nzuri za matibabu na wataalam wa hospitali hiyo.
Mkurugezi wa Huduma za Uuguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Sista Zuhura Mawona akizungumza baada ya kupokea msaada huo leo kutoka kwa Elizabeth Amandus.
Sista Mawona akiwa katika picha na baadhi ya wataalam wa Muhimbili pamoja na ndugu wa Elizabeth. Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Mkazi mmoja wa jijini Dar es Salaam ametoa msaada wa vifaa tiba aina ya (suction machines) kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kusaidia wagonjwa wenye matatizo katika mfumo wa hewa baada ya kuvutiwa na huduma nzuri za matibabu alizopatiwa mtoto wake. Mashine aina ya suction inatumiwa na wataalam wa afya kwa ajili ya kunyonya makohozi mdomoni, puani na katika koo la mgonjwa kwa lengo la kumpatia mgonjwa tiba iliyokusudiwa.
Msaada huo una thamani ya shilingi 800,000 na umetolewa leo na mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam, Elizabeth Amandus kutokana na huduma nzuri ambayo alipatiwa mtoto wake Februari 28, 2018 baada ya kumfikisha Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
Elizabeth alisema alijifungua mtoto wake katika hospitali nyingine, huku akiwa hajatimiza umri unaotakiwa (njiti) na kupewa rufaa ya kumpeleka Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi. “Wataalam wa Muhimbili walinipokea vizuri, nikahudumiwa mimi na mtoto wangu hivyo nimeamua kutoa msaada wa mashine hizi mbili ili ziwasaidie watoto wachanga wanaoletwa hapa,” amesema Bi. Elizabeth.
Akipokea msaada huo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa hospitali hiyo, Sista Zuhura Mawona amesema msaada huo umewatia moyo na kwamba wataendelea kufanya kazi kwa juhudi kubwa. “Kwa niaba ya uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, natoa shukrani kwa Elizabeth kutokana na kutambua juhudi zetu za kutoa huduma bora kwa wagonjwa, ametutia moyo kuchapa kazi kwa bidii zaidi,” amesema Sista Mawona.
No comments:
Post a Comment