Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati), akimkabidhi Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi Emmanuel Lwinga (kulia), moja ya mikono ya mashine za kufyatulia matofali zilizotolewa ili kuweza kutumika kufyatulia matofali yatakayotumika kujenga nyumba za askari ikiwa ni juhudi za serikali kutatua changamoto ya makazi kwa askari, makabidhiano hayo yamefanyika leo wilayani Korogwe, mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (aliyevaa kiraia), akisikiliza maelezo ya Ujenzi wa Nyumba za Askari kutoka kwa mmoja wa askari anaosimamia ujenzi wa nyumba hizo. Pichani ni mashine alizokabidhi Naibu Waziri ikiwa ni juhudi za serikali kutatua changamoto ya makazi kwa askari, makabidhiano hayo yamefanyika leo wilayani Korogwe, mkoani Tanga.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati), akiongozana na Viongozi wa Magereza Mkoa wa Tanga baada ya kuwasili Gereza la Kwamngumi wilayani Korogwe, Tanga kwa ziara ya kikazi.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Serikali imeyataka Magereza yote nchini kutumia Wataalamu na fursa zilizopo katika maeneo yao kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo uchache wa nyumba za askari ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli kutaka Jeshi la Magereza liimarishe shughuli za uzalishaji kwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati akikabidhi mashine za kufyatulia matofali katika Gereza la Kwamngumi Wilayani Korogwe mkoani Tanga ikiwa ni jitihada za serikali kutatua makazi ya askari nchini
Akizungumza wakati anakabidhi mashine za kufaytulia tofali kwa Uongozi wa Jeshi la Magereza mkoani Tanga, Naibu Waziri Masauni alitoa wito kwa magereza yote nchini kutumia fursa zinazowazunguka huku akiweka wazi jeshi hilo kuwa na nguvu kazi ya kutosha na wataalamu mbalimbali.
“Maagizo ya Mheshimiwa Rais Magufuli ni kuona mnatumia nguvu kazi mliyonayo ya wafungwa kuzalisha na kuweza kusimama kwa uwezo wenu wenyewe, jambo hilo linawezekaana nikiamini mna fursa kubwa ikiwemo ardhi, wataalamu na nguvu kazi,” alisema Masauni
Akizungumza katika makabidhiano hayo Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga Kamishna Msaidizi, Emmanuel Lwinga, ameiomba serikali iwasaidie katika umaliziaji wa hatua za mwisho wa nyumba hizo zitakazojengwa kwani imekua ni changamoto kubwa pindi wanapofikia mwisho wa ujenzi.
Akiishukuru Serikali kwa kuletewa mashine hizo, Mkuu wa Gereza la Kwamngumi, Mrakibu wa Magereza, Christopher Mwenda amesema watahakikisha wanatumia nguvu kazi ya wafungwa waliyonayo kutengeneza matofali imara na ameahidi mazingira ya gereza hilo kubadilika pindi ujenzi wa nyumba hizo utakapokamilika.
“Sasa tumepata vitendea kazi, awali tulikua tunapata taabu kwani tumejenga nyumba nne na ofisi moja kwa kutumia matofali ya kufyatua kwa mikono, ila kwa mashine hizo naahidi kuongeza uzalishaji wa matofali na kukaribia kumaliza tatizo la makazi wa askari katika gereza hili,” alisema Mrakibu Mwenda.
Jumla ya nyumba kumi zinatarajiwa kujengwa ndani ya mwaka huu katika Gereza hilo ikiwa ni kupambana na changamoto za makazi kwa askari wilayani Korogwe.
No comments:
Post a Comment