ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 9, 2019

Utoah azungumzia CAG kuitwa na Spika

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh

By Cledo Michael, Michael cmichael@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh amezungumzia uamuzi wa Spika Job Ndugai kumtaka CAG Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhojiwa, akisema pande hizo zinapaswa kuelewana kiutendaji ili zifanye kazi vizuri.

Utoah ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa Taasisi ya Wajibu, alisema hayo jana alipozungumza na Mwananchi lililotaka kupata mtazamo wake baada ya juzi Ndugai kumtaka Profesa Assad kufika mbele ya kamati hiyo Januari 21 kwa hiari ili kuhojiwa kuhusu madai ya kulidhalilisha Bunge, vinginevyo atapelekwa akiwa amefungwa pingu.

Utoah alisema suala hilo limeibua mjadala katika jamii na kwamba ni vyema busara ikatumika katika kulitatua kwa sababu taasisi hizo mbili zinatakiwa kufanya kazi pamoja bila malumbano.

“Spika kutaka kukutana na CAG ni suala la kawaida, lakini it’s a manner (namna) iliyofanyika. Unajua CAG analindwa sana na Katiba lakini Spika naye anasema kanuni za Bunge zinamruhusu, sasa hapo itakuwa issue (suala) ya sheria,” alisema.

Wakati Utouh aliyemwachia kiti Profesa Assad Novemba 5, 2014 akisema hayo, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amesema suala hilo watalifikisha mahakamani.

“Baada ya kushauriana na wanasheria na wabunge tumeona ni muhimu sana kwa masilahi mapana ya nchi yetu kulinda Katiba yetu,” aliandika Zitto kwenye ukurasa wake Twitter.

“Baadhi ya wabunge kutoka vyama vyote tumeamua kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya kinga ya CAG kwa mujibu wa Katiba na mamlaka ya Spika kutoa wito kwa CAG.”

Akifafanua zaidi alipozungumza na Mwananchi hasa ni lini watakwenda mahakamnani, Zitto ambaye ni kiongozi wa ACT- Wazalendo alisema, “Ndani ya wiki hii na chini ya hati ya dharura.”

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka alisema endapo CAG ataona ni vigumu kujieleza mwenyewe mbele ya kamati hiyo anaweza kwenda na mwanasheria wake.

Mwakasaka ambaye pia ni mbunge wa Tabora Mjini (CCM), alisema pamoja na kuwa CAG ni taasisi huru, lakini hayupo juu ya sheria na alichofanya Spika Ndugai kumuita mbele ya kamati ni sahihi.

Alisema kamati hiyo itakaa kama mahakama ndogo kusikiliza utetezi wa CAG na haki ya kuwa na wakili siku ya kikao.

“Ukirudi kwenye sheria hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria, hata kama una kinga na kinga ile ikasema usishtakiwe itaoanisha mambo fulani ambayo hutashtakiwa lakini siyo kila uhuru, kila mamlaka uliyopewa yana mipaka yake,” alisema Mwakasaka.

“(Kamati) inakaa kama judicial (Mahakama), ni mahakama ndogo, mtu ana haki kama anapokuwa mahakamani, unaweza ukaja na wakili sawa tu kama wewe huwezi unapohojiwa na mahakama hiyo.”

Alisema endapo Profesa Assad atashindwa kufika siku iliyopangwa ana haki ya kutoa udhuru kabla ya kukamatwa.

Alisema, “Zitto Kabwe alikamatwa aliletwa kwenye kamati. Kwa hiyo taratibu ziko hivyo, ukiingilia madaraka ya Bunge zipo kanuni ambazo utakuja uulize.”

“Kuna mipaka ya kukosoa, kuna kukosoa kwingine unaweza ukawa unamdhalilisha mtu, pale Spika hamaanishi kwamba Bunge halipaswi kukosolewa kabisa, lakini kuna taratibu zake.”

Kuhusu udhaifu wa Bunge, Mwakasaka alisema kwenye kamati za Bunge ikiwamo ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na ya Hesabu za Serikali (PAC), wapo maofisa kutoka ofisi ya CAG na wangeweza kuwasilisha mapendekezo ya ofisi yake

Kauli za wanasheria

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya sheria wamepinga uamuzi wa Spika kwamba hana mamlaka ya kumuita CAG kwenye Kamati ya Maadili huku wakishauri busara itumike.

Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alisema ibara ya 143 (6) ya Katiba inaeleza katika utekelezaji wa majukumu yake, CAG haingiliwi na mamlaka yoyote isipokuwa Mahakama pekee.

“Kama amefanya maamuzi kwa kutumia mamlaka yake anaweza kupelekwa mahakamani kwa ajili ya judicial review (taratibu za kisheria), lakini kikubwa kinachotakiwa ni kuzingatia misingi ya utawala bora,” alisema Dk Kyauke.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatuma Karume alisema suala la kulikosoa Bunge sio kulidhalilisha na kwamba Spika hawezi kumpeleka kwenye kamati hiyo mtu ambaye si mbunge.

“Kulidhalilisha (Bunge) siyo kulikosoa, huwezi kumwambia mtu ni dhaifu halafu ukasema hiyo ni kudhalilisha na kama kalidhalilisha Bunge ni nje (Bunge), mkondo wa sheria ya jinai unachukua nafasi yake siyo Bunge,” alisema.

No comments: