Ndugu jamaa na marafiki wakiwa kwenye kikao cha kujadili kuhusu kupotea kwa, Omari Athumani . Picha na
Handeni. Matukio ya kutoweka kwa wananchi sasa yanazidi kuibuka baada ya kijana mmoja mkazi wa kijiji cha Michungwani wilayani Handeni kupotea na siku chache baadaye picha zinazomuonyesha akiwa hana nguo na amevaa shanga, zikasambaa katika mitandao ya kijamii.
Kijana huyo Omari Athumani, ambaye ni dereva wa gari la mfanyabiashara aitwaye Ally Matahika, maarufu zaidi kwa jina la Kanto, alitoweka Novemba 14 mwaka jana baada ya kumuaga mama yake kuwa anakwenda kupakia mzigo wa machungwa, na hadi sasa hajaonekana.
Bado sababu za kutoweka kwake hazijajulikana, lakini mkuu wa kituo cha polisi Michungwani, Mgaza Mnkangara amesema kijana huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa tajiri yake anayeitwa Kanto na kusisitiza kwamba “mwanamke anauma”.
Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu tuhuma hizo, Kanto alisema anafahamu kuhusu kutoweka kwa Omary lakini amekataa kuzungumzia suala hilo kwa undani.
“Ni kweli,” alijibu Kanto alipoulizwa kama ana taarifa za kupotea kwa kijana huyo, lakini alipoulizwa kuhusu kudhalilishwa kwa kijana huyo na picha zake kusambaa mitandaoni, alikataa kuzungumzia suala hilo.
“Mimi kwa sasa sitaki kuzungumzia suala hilo,” alisema.
Mkuu wa wilaya, kamanda wa polisi wa wilaya na mwenyekiti wa kijiji, wote wana taarifa za kutoweka kwa Omary, lakini wameshindwa kumuhusisha tajiri wake na kitendo cha kutoweka na kudhalilishwa kwa kijana huyo na kwamba uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Akizunguymza na Mwananchi, mama mkubwa wa kijana huyo, Khadija Bakari alisema siku aliyotoweka, Omari alikwenda Kijiji cha Kwamgwe kilicho umbali wa kilomita tano kutoka Michungwani kumsalimia na akaahidi kumpa fedha za matumizi.
“Akaniambia mimi nazunguka na kazi zangu, lakini nikamuuliza ‘si unajua kuwa naumwa?’ Akasema ‘ngoja nikapakie mzigo, nikirudi tutaonana,” alisema Khadija.
Alisema huo ndio ukawa mwisho wa kuonana na mwanaye.
Anasema siku iliyofuata, akiwa njiani alimsikia mwendesha bodaboda akimwambia mwenzake aliyempakia akisema, “Kanto alichomfanyia mtoto wa watu ni kitu kibaya sana.”
Alisema katika mazungumzo hayo ndipo alipogundua kuwa mtoto wake alivishwa shanga na kudhalilishwa kwa tuhuma kuwa alitembea na mke wa mtu, habari ambayo ilimfanya apoteze fahamu.
“Nilijikuta hospitalini natibiwa. Baada ya kushtuka dada yangu akaniuliza nini kimenitokea. Nikamwambia nimesikia Omari amevalishwa shanga na kuitiwa watu. Imenichanganya,” alisema.
Alisema baadaye walifanya kikao cha wanandugu na kukubaliana waripoti tukio hilo kituo cha polisi siku iliyofuata na walipokwenda walionana na mkuu wa Kituo cha Michungwani, Mgaza Mnkangara, ambaye aliagiza mtuhumiwa akamatwe.
“Tukaambiwa tuchangie fedha za kwenda kumkamata mtu huyo. Tulitoa Sh24,000 za wakamataji. Awali (mtuhumiwa) alitaka sisi twende kwake, lakini tulipokataa akaja mwenyewe na gari lake, akaingia kwenye chumba wakajadiliana na wale polisi,” alisema.
“Baada ya maongezi yao, mkuu wa kituo akaja na kutuambia kuwa tatizo ni mtoto wetu aliyetembea na mke wa Kanto. Tukamuuliza, kama ni kweli kwa nini asingempeleka kwenye vyombo vya sheria?”
Lakini mkuu huyo wa kituo akawajibu akisema: “Wewe mama hujui uchungu wa mwanamke. Afadhali afanyiwe hivyo, sisi tulitaka auawe kabisa maana mwanamke anauma mama.”
Aliwaambia kuwa wameshazungumza na Kanto na kuwataka warudi Novemba 22, siku ambayo angemleta kijana huyo.
Siku hiyo walienda na barua ya mwenyekiti na mtendaji wa kijiji, lakini walipozikabidhi waliulizwa sababu ya kuzipeleka na walipomjibu kuwa ndivyo alivyoagiza, alizitupa, akisisitiza kuwa “mke anauma”.
Baadaye mkuu huyo aliiambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa anafahamu madai ya kupotea kijana huyo na udhalilishaji aliofanyiwa, lakini akasema suala hilo liko kwa ofisa mkuu wa upelelezi wa mkoa, ambaye angetoa taarifa zaidi.
Kamanda wa polisi wa mkoani Tanga, Edward Bukombe pia alisema analifahamu tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi.
Alipoulizwa kuwapo kwa taarifa za mtuhumiwa kuwabeza na kuwatisha ndugu wa Omari, Bukombe alisema: “Hizo taarifa tunazo ila hivyo vitu vinahitaji ushahidi. Kukiwa na ushahidi tangible (ulio dhahiri) atachukuliwa hatua. Hakuna mtu aliye juu ya sheria.”
Mpwa wa kijana huyo, Ayoub Mahiza alisema baada ya kuona wanazungushwa na polisi kijijini hapo, alimpigia simu mkuu wa wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe na kumweleza tukio hilo.
Alisema baada siku kadhaa alipigiwa simu na ofisa upelelezi wa wilaya aliyemtaka amsimulie hilo tukio na baada ya kupata maelezo alitembelea kijini hapo akiwa na timu yake ya upelelezi. Alisema watu hao walimkamata Kanto na kwenda naye Handeni.
Hata hivyo, baada ya siku tatu mtuhumiwa alirejea kijijini na walipouliza walielezwa kuwa amepewa dhamana na kwamba uchunguzi unaendelea.
“Tumeamua kushtaki kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola,” alisema Mahiza huku akionyesha nakala ya barua waliyomuandikia.
Mjomba wa kijana huyo, Sufian Mcheto alitaka mamlaka zichukue hatua.
“Inauma sana, aliyepotea si gunia bali ni binadamu,” alisema Mcheto.
Allen Michael, ambaye pia ni mjomba wa Omari, alisema kinachowaumiza ni kumuona mtuhumiwa akitamba mtaani huku akiwabeza.
“Polisi wenyewe wanatukatisha tamaa, kwa sababu mtu yuko mtaani anatamba na anatubeza akisema tutalima sana ngwe ili tumshtaki,” alisema Michael.
Mkuu wa wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alikiri kufahamu tukio hilo.
“Bahati nzuri unaongea na mwandishi wa habari mkongwe,” alisema Gondwe aliyekuwa akifanya kazi kituo cha televisheni cha ITV na pia aliyekuwa akifundisha Chuo Kikuu cha Tumaini.
“Serikali inazo taarifa na ndiyo maana unasikia polisi walifika kijijini kuchunguza. Hatuwezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu liko kwenye uchunguzi,” alisema Gondwe.
No comments:
Post a Comment