WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na wananchi wa mjini Karagwe Mkoani Kagera, katika Mkutano uliofanyika katika uwanja wa Changarawe mjini humo, leo. Lugola katika hotuba yake kwa wananchi hao, amempa wiki mbili Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, awe amefika Mikoa ya Kagera na Kigoma kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kufanya operesheni kubwa ya kuwaondoa Wahamiaji haramu katika Mikoa hiyo kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto), akimsikiliza Mkazi wa Mji wa Karagwe, Mkoani Kagera, Clemence Ishelenguzi alipokuwa anatoa kero zake mbalimbali katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Changarawe mjini humo, leo. Lugola katika hotuba yake, amempa wiki mbili Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, awe amefika Mikoa ya Kagera na Kigoma kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kufanya operesheni kubwa ya kuwaondoa Wahamiaji haramu katika Mikoa hiyo kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu. (Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).
Na Felix Mwagara, MOHA-Karagwe.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amempa wiki mbili Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI) Dkt Anna Makakara, awe amefika Mikoa ya Kagera na Kigoma kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kufanya operesheni kubwa ya kuwaondoa Wahamiaji haramu katika Mikoa hiyo kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Mji wa Karagwe katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Changarawe mjini humo, Lugola alisema kuna idadi kubwa ya wahamiaji haramu katika mikoa hiyo, hivyo CGI na Maafisa wake wahakikishe wanawaondoa wahamiaji wote haramu kupitia operesheni kubwa niliyoitangaza. “Nimepata taarifa na ndani zaidi na pia nyie wananchi hapa mmesema leo kuhusu uwepo wa wahamiaji haramu, ndio mana nimekuja hapa kwa ajili ya kuhakikisha wahamiaji hao wanaondolewa haraka iwezekanavyo hapa Kagera na Mkoa wa Kigoma,” alisema Lugola. Lugola aliongeza kuwa, licha ya kutangaza operesheni hiyo, lakini viongozi wa uhamiaji katika mikoa hiyo wawe makini mara kwa mara kuhakikisha wanawafuatilia wahamiaji hao kwa kuwashirikisha wananchi waaminifu ili waweze kutoa taarfia sahihi za wahamiaji hao.“Tunatarajia kufanya uchaguzi hivi karibuni mwaka huu, hivyo mnapaswa kuhakikisha watakaopiga kura ni Watanzania na sio wenginevyo ili kuepusha usumbufu mkubwa katika jamii,” alisema Lugola. Lugola aliwataka wananchi wa mikoa hiyo watoe ushirikiano na wasiwafiche wahamiaji hao kwasababu kumuhifadhi ni kosa kisheria, hivyo wanapaswa kuhakikisjha wanatoa taarifa za wahamiaji hao kwa maafisa uhamiaji ili waweze kukamatwa. Waziri Lugola katika mkutano huo alijibu maswali mbalimbali ya wananchi wa Karagwe yakiwemo kuhusu uwepo wa wahamiaji hao haramu ambao pia wanalalamikiwa kuwa wanatumia nguvu ya fedha kuwanyanyasa Watanzania wenye kipato kidogo. “Pia nina taarifa za kutosha kuwa, baadhi ya maafisa uhamiaji wanapewa fedha na wahamiaji hao ili wasiweze kuwakamata, sasa ole wenu, katika Serikali hii ya Magufuli haichezewi na haijaribiwi, ole wako wewe afisa uhamiaji uingie mikononi mwangu, sitakuonea huruma na hakika nitakuondoa kazini,” alisema Lugola. Lugola alisema wahamiaji haramu sio wakuchekewa hivyo amemtaka CGI ahakikishe anawapanga vizuri nmaafisa wake kwa kutembnea nyumba kwa nyumba kuwasaka na kuhakikisha wote wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka. Lugola alisema alifanya ziara katika Mkoa wa Kigoma kwa kutembelea Wilaya zote kama anavyofanya Mkoa wa Kagera, anapewa kero hiyo katika ziara hiyo, hivyo anataka Uhamiaji wawaondoa wahamiaji wote ndani ya mikoa hiyo ili Watanzania waweze kuishi kwa amani wakiendelea kujionea maendeleo ya uongozi wa Rais Dkt. Magufuli. Waziri Lugola amemaliza ziara yake Wilaya Karagwe na Wilaya inafuata ni Kyerwa, Ngara, Biharamulo na Muleba, ambapo akiwa ziara hiyo, pia uzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara pia ukutana na watumishi waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara ya Probesheni ambayo jukumu lake kuu ni kupunguza msongamano gerezani na kusimamia wafungwa waliopewa adhabu mbadala na Mahakama au wafungwa waliopata msamaha kupitia sheria ya huduma kwa jamii na kutumikia kifungo chao nje ya Gereza.
No comments:
Post a Comment