Naibu Msajili wa vyama Vya siasa Tanzania Mohamed Ali Ahmed akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu vitendo vya uvunjifu wa Sheria vinavyofanywa na mashabiki wa vyama vya Upinzani Zanzibar Ofisini kwake Mbweni Wilaya ya Magharibi B.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia maelezo ya
Naibu Msajili wa vyama vya Siasa Tanzania Mohamed Ali Ahmed alipokuwa
akizungumza katika ukumbi wa Ofisi ya Msajili ya Vyama vya siasa
Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Picha Na Miza Othman –Maelezo Zanzibar.
Na Khadja Khamis - Maelezo Zanzibar
Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Mohamed Ali Ahmed amekemea vitendo vya uvunjifu wa sheria vinavyofanya na baadhi ya wanachama wa ACT Wazalendo na waliokuwa wafuasi wa CUF wanaomuunga mkono aliyekuwa Katibu Mkuu Maalim Seif Sharifu Hamad .
Mohamed aliyasema hayo Ofisini kwake Mbweni wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu vitendo visivyo vya kiungwana baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kutoa hukumu ya Mgogoro wa viongozi kwa CUF ambapo ilimthibitisha Prof. Ibrahim Haruna Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa Chama hicho.
Alisema Ofisi ya Vyama vya Siasa haitovumilia uvunjifu wa sheria na kutumia dini katika masuala ya vyama vya siasa vinavyofanywa na mashabiki wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa Maalim Seif Sharifu Hamad.
Aliwataka wanachama na wafuasi hao kuacha kufanya vitendo vya kuchoma bendera za chama pamoja na kuhujumu mali za CUF kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria za vyama vya siasa nchini.
Aidha alisema Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa haitomvumilia chama chochote cha siasa kinachokiuka sheria ikiwemo matumizi ya dini kwa lengo la kujinufaisha kisiasa.
“Suala la kutumia dini katika harakati za kisiasa halitapewa nafasi katika zama hizi na atakayejishughulisha na vitendo hivyo atapambana na mkondo wa sheria,” alisisitiza Naibu Msajili wa vyama vya siasa.
Alisema Sheria ya vyama vya siasa inatekeleza majukumu yake ya kuhakikisha vyama vinaendeshwa katika misingi ya kistaarabu kwa lengo la kuleta maendeleo ya wananchi.
Naibu Msajili wa vyama vya siasa alitoa wito kwa wananchi na wafuasi wa vyama vya siasa kutii sheria za nchi na kutokubali kurubuniwa na wanasiasa na hatimae kujiingiza katika matatizo ambayo hayaleti tija yoyote kwa upande wao.
No comments:
Post a Comment