ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 26, 2019

Wauguzi Muhimbili watakiwa kuzingatia sheria na kanuni za kazi

 Afisa Muuguzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC),  Gustav Moyo akitoa mada kwenye kongamano la siku moja kuhusu sheria na kanuni za kazi kwa wauguzi na wakunga wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
 Baadhi ya wauguzi na wakunga wabobezi wakiwa kwenye kongamano la siku moja kuhusu sheria na kanuni za kazi kwa wauguzi na wakunga wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).



Wauguzi na wakunga Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wametakiwa kuzingatia sheria na kanuni za kazi wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa mbalimbali wanaotibiwa katika hospitali hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Afisa Muuguzi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC), Gustav Moyo kwenye kongamano la siku moja linalofanyika katika Hospitali ya Muhimbili.

Moyo aliwataka wauguzi kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia taaluma ya uuguzi na ukunga inayoitwa “The Nursing and Midwifery Act. 2010” pamoja na kanuni zake.

Pia, aliwataka wauguzi na wakunga kutowatelekeza wagonjwa wakati wanapohitaji huduma kwa kuwa kumtelekeza mgonjwa ni kosa kwa mujibu wa sheria na hivyo amewataka kuzingatia sheria na kanuni za kazi ili kuboresha huduma mahali pa kazi.

“Wauguzi na wakunga mnapaswa kuzingatia upendo na huruma kwa wagonjwa, ndugu na jamaa wa wagonjwa. Jambo muhimu mnatakiwa kuboresha mawasiliano na kuzingatia maandili na kuwaona ndugu wa wagonjwa ni wadau,” amesema Moyo.

Naye  Happy Masenga katika kongamano hilo alisisitiza umuhimu wa wauguzi na wakunga kujiendeleza katika mafunzo mbalimbali ili kuendana na sayansi na teknolojia wakati wa kutoa huduma.

Katika mafunzo hayo pia wamefundishwa jinsi ya kujaza kitabu maalamu (Log Book) ambacho kinasaidia upatikanaji wa leseni kwa wauguzi. Watoa mada katika kongamano hilo ni Gustav Moyo, Happy Masenga na Asha Gembe.

No comments: