ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 26, 2019

TABORA YAGUNDUA WAGONJWA 2,369 KATI YA 2,850 WA TB WALIOKUSUDIWA MWAKA JANA

 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri(kulia) , Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu(katikati) na Mganga wa Mkoa wa Tabora Dkt. Honoratha Rutatinisibwa(kshoto) wakijadiliana wakati wa maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani kwa mwaka 2019 ambapo kimkoa yamefanyika wilayani Nzega ambayo kauli mbiu inasema wakati ni huu .tuunganishe nguvu katika kutokomeza kifuaa kikuu.
 Mganga wa Mkoa wa Tabora Dkt. Honoratha Rutatinisibwa akitoa maelezo kuhusu hali ya kifua kikuu mkoani Tabora wakati wa maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani kwa mwaka 2019 ambayo kimkoa yamefanyika wilayani Nzega.
 Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifuaa Kikuu na Ukoma(NTLP) Dkt. Liberate Mleo akitoa maelezo kuhusu hali ya kifua kikuu nchini wakati wa maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani kwa mwaka 2019 ambapo Tabora kimkoa yamefanyika wilayani Nzega.
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Msalika Makungu akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuwahutubia wananchi wakati wa maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani kwa mwaka 2019 ambayo kimkoa yamefanyika wilayani Nzega.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akiwahutubia wananchi wakati wa maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani kwa mwaka 2019 ambayo kimkoa yamefanyika wilayani Nzega.
Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Nzega wakiwasikiliza viongozi mbalimbali wakati wa maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani kwa mwaka 2019 ambayo kimkoa yamefanyika wilayani Nzega. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema wakati ni huu tuunganishe nguvu katika kutokomeza kifuaa kikuu. Picha na Tiganya Vincent

MKOA wa Tabora ulilenga kugundua wagonjwa wa kifua kikuu ,2850 kwa mwaka 2018 lakini ulifanikiwa kugundua wagonjwa 2,369 wa kifua kikuu ikiwa sawa na asilimia 83 ya malengo uliojiwekea.

Kauli hiyo imetolewa mjini Nzega na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati wa maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani kwa mwaka 2019 ambapo kimkoa yamefanyika wilayani Nzega.

Alisema sababu ambazo zilisababisha kutoweza kufikia malengo hayo ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu kifua kikuu na uchache wa vituo vya tiba vinavyoweza kupima na kudhibitisha ugonjwa kifua kikuu.

Mwanri alisema juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisa wanatafuta wagonjwa wote wa kifua kikuu na kuwaweka kwenye matibabu sahihi.

Alisema elimu sahihi juu ya kifua kikuu, uimarishaji wa huduma za kifua kikuu na kubadili tabia vinhitajika kwa kiwango kikubwa, ili wananchi waweze kujua dalili mapema na kutumia huduma za afya.

Mwanri alitoa wito kwa wadau wote wa afya na wasio wa afya kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya kifua kikuu, uhamasishaji unaolenga kubadili tabia pamoja na watoa huduma kuungana pamoja ili kuhakikisha elimu kuhusu kifua kikuu inatolewa na huduma za kifua kikuu zinapatikana kiurahisi.

Naye Mganga wa Mkoa wa Tabora(RMO) Dkt. Honoratha Rutatinisibwa alisema lengo la maadhimisho haya ni kukumbusha, kuelimisha na kushirikisha jamii katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, na hivyo kuongeza uibuaji wa wagonjwa wa Kifua Kikuu, kuwapatia matibabu na hivyo kupunguza na kutokomeza ugonjwa huu wa hatari unao sababisha vifo vya watu wengi.

Alisema Mkoa wa Tabora suala la uibuaji wa wagonjwa Kifua Kikuu unaongezeka kila mwaka ambapo takwimu zinaonesha idadi ya wagonjwa walioibuliwa imeongezeka kutoka 1,751 kwa mwaka 2014 hadi 2,369 kati ya lengo la kwa mwaka 2018.

Dkt. Rutatinisibwa alisema kiwango cha maambukizi ya Kifua Kikuu kwa takwimu za 2018 kwa mkoa wa Tabora ni wagonjwa 269 kwa kila watu laki moja hivyo kuwa na makadirio ya wagonjwa 7000.

Aliongeza kuwa huduma shirikishi za Kifua Kikuu na VVU zinaendelea kutolewa ambapo kwa mwaka 2018 idadi ya wagonjwa wa Kifua Kifuu 2,271 sawa na asilimia 95.9 walipimwa VVU kati ya hao 837 sawa na asilimia 36.9 walikutwa na maambukizi ya VVU na wote walianzishiwa dawa za kufubaza VVU.


Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya kifua kikuu mwaka huu ni wakati ni huu tuunganishe nguvu katika kutokomeza kifua kikuu.

No comments: