ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 29, 2019

TANZANIA YANG'ARA BENKI YA DUNIA

Mwenyekiti wa Kampuni ya Mipangomiiji ya HUSEA na Makamu wa Rais wa Chama cha Wataalam wa Mipango Miji nchini, Bwana Renny Chiwa
Na. Mwandishi Wetu, Washington DC Marekani

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa katika kukabiliana na tatizo la makazi holela duniani.

Takwimu zinaonyesha zaidi ya watu bilioni 1 kati ya bilioni 7.4 duniani wanaishi katika makazi holela bila kuwa na umiliki halali wa maeneo yao huku wakikabiliwa pia na hali duni ya miundombinu, uhaba wa huduma za kijamii na migogoro sugu ya ardhi.

Hata hivyo, hatua ya serikali ya Tanzania kushirikisha sekta binafsi katika kupangilia miji, kupima viwanja na kumilikisha ardhi kwa hatimiliki imeleta tija na kuongeza kasi kubwa katika kurasimisha na kuboresha makazi holela nchini.

Hayo yameelezwa na Mratibu Mwandamizi wa Miradi wa Kampuni ya Mipango Miji ya HUSEA, Bwana Edward Kinabo, katika Mkutano Mkuu wa Benki ya Dunia unaohusu Ardhi na Umaskini, unaoendelea jijini Washington nchini Marekani.

Akiwasilisha mada jana, kwa niaba ya Kampuni ya HUSEA iliyohusu *Mafanikio ya Ubia baina ya Sekta Binafsi na Jamii katika Kurasimisha Makazi kwa kutumia fedha zinazochangwa na Wananchi wenyewe* Kinabo alisema kwa miaka mingi ongezeko la idadi ya watu na ukuaji wa kasi wa miji dhidi ya uhaba wa bajeti, nguvu kazi na vitendea kazi, vilisababisha kuwepo kwa kasi ndogo ya upangaji miji na hivyo kukithiri kwa makazi holela mijini kwa zaidi ya asilimia 70.

Hata hivyo, alifafanua kuwa kupitia mazoezi shirikishi ya kuchangia gharama yanayotekelezwa na kampuni binafsi sasa maelfu ya wananchi wanapata fursa ya kumiliki maeneo yao kisheria.

*Hatua ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushirikisha kampuni binafsi imeleta tija na kasi kubwa katika kukabiliana na makazi holela nchini*

Tunampongeza Waziri wetu wa Ardhi kwa uamuzi sahihi wa kushirikisha sekta binafsi na kuwa mhamasishaji mkuu wa urasimishaji wa makazi…jitihada hizi zimeleta tija na kasi kubwa
 alisema Kinabo.

Mkutano huo wa Benki ya Dunia unashirikisha wadau wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo viongozi na maafisa wa serikali, Asasi za Kiraia na wawakilishi kutoka sekta binafsi wakiwemo watoa mada walioalikwa kutoa uzoefu juu ya namna bora ya kushughulikia masuala yahusuyo ardhi na umasikini.

Akifafanua kuhusu kasi ya urasimishaji makazi nchini, Kinabo alisema Kampuni ya HUSEA pekee imeweza kuandaa ramani za mipango miji na kuratibu upimaji wa zaidi ya viwanja 30,000 katika mitaa mbalimbali ya Manispaa za Ubungo, Kinondoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam, huku Kampuni hiyo ikiwa katika hatua za awali za kufanya kazi kubwa zaidi katika Jiji la Mbeya, Arusha na mkoa wa Songwe.

Alisema takwimu za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinaonyesha kuwa hadi kufikia Mwezi Mei mwaka 2017 tayari kulikuwa na jumla ya kampuni za mipango miji 40 na za upimaji 67 zilizosajiliwa huku nyingi kati ya hizo zikijihusisha na mazoezi ya urasimishaji makazi.

Kwa kasi hii, tunaamini ndani ya miaka michache ijayo tathmini zitaonyesha kupungua kwa makazi holela nchini

Alisema urasimishaji makazi ni jitihada muhimu katika kufufua mitaji mfu ya ardhi, kuongeza usalama na thamani ya miliki za wananchi na hivyo kuwawezesha kuvutia mitaji, kupunguza umaskini na kuchochea maendeleo yao.

Tunaifanya kazi hii bila kutegemea fedha za wafadhili wa nje wala bajeti ya serikali. Tunaifanya kazi hii kwa nguvu ya wananchi wenyewe… kwa kuwaelimisha, kuwashirikisha na kuwahamasisha kuchangia gharama nafuu za kurasimisha maeneo yao

Alisema mfumo wa uchangiaji gharama unampa mwananchi unafuu wa zaidi ya asilimia 90 ya gharama ambazo angelazimika kuzibeba zote kama angepima eneo lake peke yake.

Awali, akichambua takwimu za hali halisi ya nchi kuhusu ongezeko la watu na makazi holela, Kinabo alisema Ripoti ya Hali ya Maendeleo ya Binadamu Tanzania iliyotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) mwaka 2017, inaonyesha idadi ya watu nchini inaongezeka kwa zaidi ya asilimia 2.7, sawa na ongezeko la watu milioni 1.2 kwa mwaka.

Alisema kasi hiyo, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 67 ifikapo mwaka 2025 na watu milioni 89.2 ifikapo mwaka 2035.

Aliuambia mkutano huo kuwa Tanzania ina kasi kubwa ya ongezeko la watu mijini ambayo ni asilimia 5.2 kwa mwaka, kiwango ambacho ni zaidi ya mara mbili ya wastani wa dunia ambao ni asilimia 2.1 na zaidi ya wastani wa Afrika ambao ni asilimia 3.5.

Aidha, akinukuu Ripoti ya Shirika la Makazi Duniani (UN Habita) ya mwaka 2016 kuhusu Ukuaji wa Majiji, alisema wakati theluthi mbili ya watu wote duniani watakuwa wanaishi mijini ifikapo mwaka 2050, huku asilimia 90 wakitarajiwa kutokea ndani ya Bara la Afrika na Asia, Tanzania itakuwa ni nchi ya tisa kwa kuwa watu wengi waishio mijini, ikitanguliwa na India, China, Indonesia, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

*Kwa kadri idadi ya watu inavyozidi kuongezeka mijini kuliko vijijini ndivyo kiini cha umaskini wa dunia kinavyozidi kuhamia mijini kutoka vijijini. Ile dhana iliyozoeleka kuwa umaskini umekithiri vijijini tu sasa imepitwa na wakati* alisema Kinabo

Mbali na urasimishaji wa makazi holela, Mtaalam huyo wa Miradi pia amezishauri nchi zinazoendelea kufanya mageuzi makubwa ya mwelekeo wa kisera ili kutatua changamoto mpya ya umaskini unaozidi kukithiri zaidi mijini kuliko vijijini.

Kwa kufanya hivyo ndio tutaweza kuharakisha jitihada za kutimiza lengo la kutokomeza aina zote za umaskini kila mahali duniani ifikapo mwaka 2030, kama ilivyoazimiwa katika Shabaha za Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yanayotekelezwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwemo Tanzania alisisitiza Kinabo.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Kampuni ya Mipangomiiji ya HUSEA na Makamu wa Rais wa Chama cha Wataalam wa Mipango Miji nchini, Bwana Renny Chiwa.

Mkutano huo ulioanza Tarehe 25 unatarajiwa kumalizika Tarehe 29 Machi mwaka 2019.

No comments: