Saturday, March 30, 2019

TOFAUTI YA JOKATE MSANII NA DC JOKATE MWEGELO!

ALIJULIKANA kama Jokate Mwegelo aliyeibuliwa na Miss Tanzania mwaka 2006 ambapo alichukua namba 2 akitokea Kanda ya Temeke. Baada ya hapo akawa msanii wa filamu za Kibongo na kupata jina kubwa.

Mlimbwende huyo hakukomea hapo, akaendeleza kipaji chake cha mitindo na kufungua kampuni yake Kidoti Loving. Jokate ni mjasiriamali na anayependa kufanya kazi za kijamii. Ndani ya moyo wake ana kiu ya kusaidia na kuwatumikia watu, jambo ambalo alilionyesha tangu mapema kabisa.

Kuna wakati aliingia kidogo kwenye muziki wa Bongo Fleva na akashiri kishwa na AY (Ambwene Yesaya) katika kibao Kings & Queens kisha baadaye akaachia kibao chake ‘Leo Leo’ alichofanya kolabo na Ice Prince kutoka Nigeria.

Anavyo vipaji vingi, lakini ukweli utaendelea kubaki kuwa Miss Tanzania ndiyo iliyomtoa. Alitokea Miss Tanzania iliyopata kuwa maarufu zaidi kuliko shindano la mwaka mwingine wowote. Ni mwaka ambao washiriki wake karibu wote wa juu (Top 5) wameendelea kung’ara mpaka sasa.

Akiwa namba mbili, alitanguliwa na Wema Sepetu (Miss Tanzania), staa wa filamu anayetesa kwa sasa, kisha nyuma yake Lisa Jensen ambaye naye aliangukia kwenye filamu za Kibongo, ingawa hakung’aa sana, Sarah Kangezi (namba 4) na Irene Uwoya (namba 5) ambaye habari yake kwenye sinema za Kibongo inajulikana!

Ukiangalia utaona kuwa warembo wote hao, pamoja na mambo mengine, kwanza walianzia kwenye filamu. Mfano Jokate na Lisa wao walipata kuigiza katika filamu moja iitwayo Fake Pastors ambayo ndani yake kuna Vincent Kigosi ‘Ray’, Adam Kuambiana (marehemu) na wasanii wengineo.

Kwa sasa huwezi kutaja jina lake bila utangulizi wa aidha Mhe. DC Jokate Mwegelo au DC Jokate. Yes! Ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani. Kama mwandishi wa burudani kwa zaidi ya muongo mmoja sasa, namfahamu vizuri DC Jokate kwa kiasi chake. Wakati anashiriki Miss Tanzania 2006, nilikuwa nina miaka miwili kwenye uandishi wa habari.

Inafahamika kuwa huko nyuma ilikuwa vigumu kuwaaminisha wengi kuwa mashindano ya urembo siyo uhuni. Mbaya zaidi, hata baada ya mashindano yenyewe kupita, washiriki wake walihusishwa katika skendo mbalimbali. Kwa Jokate ni tofauti.

Anajua anafanya nini katika jamii yake. Mara kadhaa alionekana kwenye shughuli za kijamii akiwasaidia wanawake na vijana hasa watoto wa kike. Mara paaap! Julai, mwaka jana akateuliwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa DC.

Baadhi ya watu wakahofu. Jokate anaweza kuwa mkuu wa wilaya kweli? Wakiangalia alipotoka kwenye Miss Tanzania, Bongo Muvi nk, wakakosa imani. Mimi namfahamu Jokate kama mpambanaji, mwenye akili nyingi na mbunifu. Hivyo, sikuwa na shaka hata kidogo na uteuzi wake. Nilijua ataitumia vyema talanta yake ya uongozi iliyoanza kuonekana ndani yake muda mrefu

Mara kadhaa nimepata kuonana na DC Jokate kabla ya kuwa mkuu wa wilaya. Hiyo ni kwa sababu kazi zetu zinahusiana. Nakumbuka mara ya mwisho nilikutana naye Mwanza mwaka 2016 katika Viwanja vya Rocky City Mall kwenye Fainali za Miss Tanzania, yeye akiwa mmoja wa washereheshaji.

Baada ya kumalizika kwa shindano hilo, mashabiki wake wengi walitaka kupiga naye picha. Nilipanda jukwaani nikitaka kufanya naye interview fupi lakini haikuwezekana kutokana na namna watu walivyokuwa wakimzonga.

Baada ya hapo sikuwahi kuonana naye tena, hadi juzi Jumanne wiki hii, alipokuja ofisini kwetu, Sinza – Mori kama mkuu wa wilaya! Aliyekuwa mbele yangu alikuwa Jokate mwingine kabisa. Ndiyo! alikuwa DC Jokate mwenye kujiamini, anayejielewa zaidi na mwenye fikra mpya kuhusu maendeleo na uongozi. Jokate amekuwa mwingine kuanzia mavazi, namna anavyozungumza na kufafanua mambo. Utaona kabisa, kichwa chake kimejaa madini. Naweza kumfananisha Jokate na mgodi unaotembea.

DC JOKATE WA MIPANGO

Jokate anamudu na anaonekana kutimiza majukumu yake vyema. Ukimfuatilia kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii, utamuona mara nyingi akiwa saiti kukagua na kushughulikia kero mbalimbali za wananchi. Kiu yake inaonekana wazi kudhamiria kubadilisha Kisarawe. Mipango yake inadhihirisha hilo na hata namna anavyofanya kazi ni ushahidi tosha.

TOKOMEZA ZIRO


Pamoja na mambo mengi mazuri ambayo DC Jokate amefanya katika kipindi kifupi kisichofika mwaka mmoja katika wilaya yake, tayari ana mkakati wa kupandisha elimu wilayani mwake kupitia kampeni aliyoipa jina la Tokomeza Ziro.

Kampeni hiyo ina lengo la kupeleka maendeleo ya elimu katika Wilaya ya Kisarawe. Kampeni hiyo itafanyika leo Jumamosi, katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Makamu wa Rais wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan.

Jokate alisema, lengo la kampeni hiyo ni kukusanya fedha zitakazosaidia ujenzi wa shule ya wasichana ya Kisarawe, mkoani Pwani. Alisema: “Tokomeza Ziro ni kampeni ya kuhakikisha tunapanua elimu wilayani Kisarawe na tunaanza kwa kujenga shule hiyo ya wasichana. Nawaomba watu wote wenye kutaka maendeleo ya Kisarawe wajitokeze kwa wingi pale Milimani City Jumamosi (leo).”

“Kuna changamoto nyingi Kisarewe, lakini la elimu nimeona nilipe kipaumbele kwanza, mengine yatafuata. Zipo changamoto nyingi kwenye elimu kama mimba za utotoni, lakini tukijenga mabweni tutakuwa tumepunguza tatizo kwa kiasi kikubwa,” alisema DC Jokate.

Katika kufanikisha hilo, DC Jokate alisema wadau wajitokeze kuingia kwa wingi kwa mchango wa Tsh. Milioni 1 kwa meza moja. Huu mwanzo wa mapambano ya DC Jokate Mwegelo katika kufanikisha maendeleo ya Kisarawe. Wadau tujitokeze kwa wingi, tumuunge mkono!

No comments: