Gari zilizobeba makontena yenye tani 126 za Samaki na Maziwa yakiwa yameegeshwa katika jaa la Kibele Wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Baadhi ya maboksi ya Samaki walioharibika yakiwa kwenye Kontena yakisubiri kushushwa kwa ajili ya kuharibiwa katika eneo la Kibele Wilaya ya Kati Unguja.
Gari aina ya Gurdoza la Manispaa ya Mjini likisaga Samaki na Maziwa yaliyoharibika katika eneo la la Kibele Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini Unguja.
Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Athari za Chakula wa
ZFDA Aisha Suleiman akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
kuangamizwa tani 126 za Samaki na Maziwa kutokana na kutokufaa kwa
matumizi ya binadamu.
Picha na Makame Mshenga.
Na Ramadhani Ali Maelezo Zanzibar
Wakala wa Chukula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imeteketeza samaki tani 106 aina ya peduu walioingizwza nchini kutoka China na maziwa tani 23 kutoka Dubai baada ya bidhaa hizo kuharibika na kukosa sifa kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Samaki hao waliokuwa kwenye makontena manne ya futi 40 waliingizwa na Kampuni ya Drive Shark na kontena moja la maziwa kutoka Dubai yaliletwa na mfanyabiashara Yunus Hashim.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuangamiza bidhaa hizo katika kijijii cha Kibele, Afisa Uhusiano wa ZFDA Abdulmatin Yassin alisema samaki waliharibika baada ya kukosa umeme wa uhakika kwenye makontena.
Alisema kukosekana kwa umeme wa kutosha kwenye makontena yalipofika bandarini Zanzibar kulisababisha kupungua barafu iliyogandisha samaki na kuanza kuharibika.
Abdulmatin alisema samaki wanapoingizwa nchini huwa wameganda na hutakiwa waendelee kubakia katika barafu wakati wote lakini wakati makontena yakisubiri taratibu za uingizaji palitokea kasoro na kusababisha samaki kuharibika.
Alisema kwa upande wa bidhaa ya maziwa, yaliharibika baada ya baadhi ya maboksi kupasuka wakati yakisafirishwa kutoka Dubai kuja Zanzibar.
Mkuu wa Kitengo cha uchunguzi wa athari zitokanazo na chakula wa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar Aisha Suleiman alisema samaki aina ya peduu wanaoingia nchini kutoka nje ni salama kwa matumizi ya binadamu lakini umakini unahitaji wakati wa kuwasafirisha na wanapofika bandarini .
Aliwataka wananchi wanaponunua samaki wanaoingizwa nchini kuwa waangalifu na wahakikishe wameganda kwenye barafu na wasiwaweka muda mrefu kabla ya kuwapika ama waendelee kuwaweka katika barafu.
Aidha aliwashauri wafanyabiashara kufuata taratibu zote za kuingiza bidhaa nchini na kutafuta bidhaa zenye ubora uliowekwa na Bodi ya Chakula na Dawa Zanzibar ili kujiepusha na gharama zisizokuwa za lazima.
Alikumbusha kuwa Sheria ya ZFDA kwa bidhaa zilizoharibika ama kupitwa na muda wa matumizi, mfanyabiashara hushauriwa kuirudisha ilikotoka ama kuangamizwa kwa gharama zake.
Mkuu huyo wa Kitengo cha uchunguzi wa athari zitokanazo na chakula wa ZFDA amewahakikishia wafanyabiashara kwamba Bodi hiyo haina ni ya kuwadidimiza kutokana kazi nzuri wanayofanya, lakini lengo ni kulinda afya za wananchi kwa kuhakikisha wanapata bidhaa zilizo salama.
Mmoja wa Afisa kutoka Kampuni ya Drive Shark, alieficha jina lake, aliishauri Serikali kwa kushirikiana na mfanyabiashara husika kuangalia matumizi mbadala wa bidhaa za aina hiyo, kwa sababu hazina sumu, badala ya kupoteza fedha nyingi kuziangamiza.
No comments:
Post a Comment