Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Jason Rweikiza (Mb) akizungumza na wananchi na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa kijiji cha Namela Manispaa ya Mtwara wakati wa ziara ya kamati yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Mtwara.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiwahimiza wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kuzitumia vizuri ruzuku wanayoipata.
Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa kijiji cha Namela Manispaa ya Mtwara wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Jason Rweikiza (Mb) alipokuwa akizungumza nao kuhusu umuhimu wa TASAF wakati wa ziara ya kamati yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Mtwara.
Wakurugenzi Watendaji katika halmashauri za wilaya nchini wametakiwa kuhakikisha wanasimamia vema fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini zinawafikia walengwa kama ilivyokusudiwa. Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Jason Rweikiza (Mb) wakati wa ziara ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo mkoani Mtwara ikiwa ni pamoja na kujiridhisha namna Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unavyotekelezwa.
Mhe. Rweikiza amekemea tabia ya baadhi ya Wakurugenzi Watendaji katika halmashauri kuelekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika matumizi mengine badala ya kuwanufaisha walengwa ambao ni kaya maskini na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja.
“Wakurugenzi Watendaji, mnao wajibu wa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha maisha ya kaya maskini zote nchini kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini,” Mhe. Rweikiza amesisitiza.
Aidha, amewapongeza wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa kijiji cha Namela, Manispaa ya Mtwara kwa kutumia vizuri ruzuku wanayopata katika kuboresha maisha yao ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za kisasa na kujishughulisha na ufugaji wa mbuzi na kuku. Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amewataka wanufaika wa Mpango kuendelea kutumia vema ruzuku wanayopata ili waweze kuondokana na umaskini.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewaasa wanufaika hao kuwekeza ruzuku hiyo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazowaongezea kipato na kuondokana na umaskini. Kwa upande wao, wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kijiji cha Namela, wameishukuru Serikali kuwawezesha kupitia TASAF kwani wameweza kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.
Mmoja wa wanufaika hao, Bw. Abdallah Chingwalu amesema, ametumia ruzuku aliyoipata kujenga nyumba ya kisasa, kununua mbuzi wawili ambao amewafuga na kufikia mbuzi 17, kufuga kuku ambao wamefikia 20 hivi sasa. Mnufaika mwingine, Bi. Fatuma Shamte, ametoa ushuhuda kuwa, ruzuku anayoipata imemsaidia kupata milo mitatu kwa siku tofauti na awali, kusomesha wajukuu na kufanya ukarabati nyumba yake ambayo haikuwa katika hali nzuri.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umelenga kuziwezesha kaya zote maskini kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu katika kuendesha maisha ya kila siku.
No comments:
Post a Comment