ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 18, 2019

Shirika la Sun Flower kujenga kiwanda nchini

 Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na uzalishaji wa Kilimo cha Alizeti (Sun Flower) la Alemdar Bwana Oktay Alemder Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika na Ujumbe wake kwa mazungumzo. Kati kati yao ni Mwakilishi wa Shirika hilo hapa Zanzibar Bibi Batuli. 
 Mkuu wa Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na uzalishaji wa Kilimo cha Alizeti (Sun Flower) la Alemdar Bibi Fatma Atala Kushoto akitoa maelezo ya utendaji wa Shirika lake kwa Balozi Seif.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Shirika la Alemdar kutoka Nchini Uturuki Afisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
 Baadhi ya Viongozi wa Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na uzalishaji wa Kilimo cha Alizeti (Sun Flower) la Alemdar wa Uturuki na wale waliopo Zanzibar wakifuatilia mazungumzo yao na Balozi Seif hayupo pichani. Picha na – OMPR – ZNZ.

Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na uzalishaji wa Kilimo cha Alizeti {Sun Flower } la Alemdar kutoka Nchini Uturuki limeonyesha nia ya kutaka kujenga kiwanda kitakachozalisha Bidhaa tofauti kwa kutumia malighafi ya Maua hayo katika azma ya kuitikia wito wa Serikali wa kuwa Nchi ya Viwanda katika kipindi kifupi kijacho.

Ofisa Mkuu wa Shirika hilo Bibi Fatma Atala alieleza hayo wakati Ujumbe wa Viongozi wa Shirika hilo ulioongozwa na Mwenyekiti wake Bwana Oktay Alemder ulipokutana kwa mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Bibi Fatma Atala alisema Mradi huo wa Kibiashara endapo utafanikiwa kuanzishwa Visiwani Zanzibar unalenga pia kuwashirikisha moja kwa moja Wakulima Vijini kwa kulima Maua ya Alizeti katika baadhi ya maeneo yao ya Kilimo.

Alisema Maua ya Alizeti ni bidhaa inayoendelea kuwa na hadhi kubwa katika masoko ya Kimataifa ambayo inaweza kusaidia kunyanyua mapato ya washiriki katika ukulima wake sambamba na kuongeza Mapato ya Taifa.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alueleza Ujumbe huo wa Viongozi wa Shirika la Alemdar kutoka Nchini Uturuki kwamba Tanzania tayari imeshaamua kuwa Nchi ya Viwanda ifikapo Mwaka 2025.

Balozi Seif alisema Wawekezaji wa ndani na nje ya Nchi wana fursa ya kuitumia nafasi hiyo katika Ushiriki wao wa Uwekezaji utakaokwenda sambamba na azma hiyo ya Serikali.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Ujumbe huo unapaswa kuzingatia zaidi mazingira halisi ya Zanzibar yanayoendelea kukumbwa na changamoto la ufinyu wa Ardhi.

Balozi Seif aliushauri Ujumbe wa Viongozi hao kutayarisha maombi na kuyawasilisha kwa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA} kwa hatua ya kuangalia uwezekano wa kuufanyia uchambuzi yakinifu Mradi wao na mazingira halisi ya Ardhi yaliyopo Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Ujumbe huo wa Viongozi wa Shirika la Alemdar kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari muda wowote kuunga mkono jitihada za Shirika hilo za kutaka kuitumia fursa ya Uwekezaji Vitega Uchumi iliyopo Nchini Tanzania.

No comments: