ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 15, 2019

WANAWAKE WANAOJISHUGHULISHA NA UVUVI NCHINI WAUNDA MTANDAO WAO UJULIKANAO ‘TAWFA’



Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Rashid Tamatama akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi  Mtandao wa Wawanawake  wanaojishughulisha na  Shughuli za uvuvi  nchini ujulikanao kama  (Tanzania Women Fish Workers Association-TAWFA) mtandao ambao utasaidia kuwezesha masoko na fursa za kiuchumi. Wanawake wanaoshuhudia ni baadhi ya wajumbe ni viongozi wa muda wa Mtandao huo.



KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Rashid Tamatama amezindua rasmi Mtandao wa Wawanawake  wanaojishughulisha na  Shughuli za uvuvi  nchini ujulikanao kama  (Tanzania Women Fish Workers Association-TAWFA) mtandao ambao utasaidia kuwezesha masoko na fursa za kiuchumi.

Tukio hilo limefanyika mapema leo Aprili 15, Jijini Dar es  Salaam huku zaidi ya wajumbe 100 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.

Awali akifungu na kuzindua mtandao huo, Dk. Rashid alieleza kuwa Serikali imekuwa na mipango mbalimbali ya kuinua Wanawake kiuchumi ambapo imeweza kuwakutanisha wanawake hao nchinikote kuwa kiunganiko cha Taasisi binafsi na Wizara.

“Wizara kupitia idara ya uvuvi tokea 2017, imekuwa ikitekeleza mradi wa miongozo ya hiyari ya kuhakiki shughuli za uvuvi mdogo unakuwa endelevu katika kuongeza chakula na kupambana na umasikini mradi ambao umefadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Kimataifa (FAO) pamoja na serikali yetu.
TAWFA kwa sasa ni chombo cha kuwaunganisha pamoja na kuwatafutia masoko ya pamoja kuanzia ngazi ya chini mpaka hatua ya juu” alieleza Dk. Rashid.

Aidha, ameongeza Wanawake wengi nchini wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi idadi imeendelea kuongezeka siku hadi siku na TAWFA itakuwa muhimili thabiti.

"Wanawake wamekuwa wakifanya shughuli za uvuvi kwa kiwango kikubwa na chombo hiki kitakuwa chombo kitakachowasaidia kufanya shughuli zao hizi kwa pamoja." Alisema.

Pia amebainisha kuwa, wanawake wengi wamekuwa wakilalamikia mitaji na kuomba kuwezeshwa zaidi.
Dk. Rashid amemalizia kuwa, kwa sasa wameanzisha dawati maalum la wajasiriamali waliopo kwenye sekta ya uvuvi na kwa sasa wameanza na wale wafugaji wa samaki wa kwenye vizimba ambao wameunganishwa kwenye benki ya kilimo hivyo kwa mpango wa sasa pia kuona namna ya kuwaingiza na  TAWFA  ili wapate kuimalisha masoko yao.

Aidha, Dk. Rashid ametoa wito kwa Wanawake wanao fanya shughuli za uvuvi na kuchakata mazao ya uvuvi kutumia chama chao kuweza kupanua fursa ya masoko baina ya wao kwa wao kutokana na sehemu wanazotoka.

Nae Mtendaji mkuu wa  Shirika la usimamizi mazingira na maendeleo Tanzania ( EMEDO), Bi.Editrudith Lukanga ambaye pia ni mwanzilishi wa TAWFA amewashukuru Wanawake wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi nchini kwa kujitokeza na kuunda mtandao huo wenye lengo la kuwaleta pamoja katika shughuli za kimaendeleo.

“Kwa Tanzania wanawake wanaojishughulisha na uvuvi wanakaribia kufikia asilimia 50, hii inaongeza fursa zaidi kwetu wanawake na kuona tunaendelea kujitokeza zaidi kwenye shughuli za uzalishaji mali kupitia uvuvi” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa maendeleo ya uvuvi kutoka Wizara ya mifugo na uvuvi, Magese Emmanuel amesema kuwa, wananchi  zaidi ya milioni 20 wanaoishi pembezoni mwa maeneo ya maji hufaidika  kutokana na uvuvi wakiwemo wanawake ambao wamekuwa wakifanya shughuli hizo za kila siku.

Mkutano huo wa siku mbili wa TAWFA ni wa kwanza kufanyika nchini ambapo wajumbe zaidi ya 100 wamepata kupitia katiba na madokezo mbalimbali ikiwemo pia uwasilishwaji wa mada zilizotolewa na washirika na wadau ikiwemo kutoka Wizara ya uvuvi nchini













No comments: