ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 18, 2019

ASKARI WA DHAHABU MWANZA WAACHIWA HURU, RPC AFUNGUKA! July 18, 2019 by Global Publishers


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mwanza leo Alhamisi Julai 18, 2019, imewaachia huru askari wanane wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza ambao walituhumiwa kwa kosa la kupokea na kuomba rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wa dhahabu Januari mwaka huu.

Wakili Mkuu wa Serikali, Castus Ndamugoba, ametumia kifungu kifungu 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 na marekebisho ya mwaka 2002 kuawaachiwa huru askari polisi wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kusafirisha kilo 319 za dhahabu na Sh305 milioni ambapo aliieleza mahakama hiyo kuwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) haina haja ya kuendelea na shauri hilo.

Kutokana na ombi hilo la Jamhuri, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mwanza, Rhoda Ngimilanga, aliyekuwa akisikiliza shauri hilo namba 1/2019 aliifuta na kuwaachia huru washtakiwa ambao kwa pamoja waliondoka mahakamani wakitumia gari moja aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe.

Wafanyabiashara wanne wa dhahabu, Hassan Sadiq, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda na Sajid Hassan walioshtakiwa pamoja na askari hao walikiri mashtaka dhidi yao na kuhukumiwa vifungo kati ya miaka mitano hadi 15 au faini kati ya Sh5 milioni hadi Sh100 milioni.

Wafanyabiashara hao walilipa zaidi ya Sh529.8 milioni kukwepa kwenda jela..

GPL

No comments: