Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema siku akikutana wa Rais wa Tanzania, John Magufuli atamueleza jinsi viongozi aliowateua walivyojaa hofu na kushindwa kufanya uamuzi.
Lema aliyesimamishwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge kutokana na kuunga mkono kauli ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuwa Bunge la Tanzania ni dhaifu, ametoa kauli hiyo jana jioni Jumanne Julai 2, 2019 katika mkutano wa hadhara.
Amesema hofu hiyo inawafanya viongozi kushindwa kufanya uamuzi, kwamba hofu hiyo sasa imewakumba hadi wanasiasa ambao baadhi wanalazimika kuhama vyama vyao na kutokuwa wa kweli.
Amesema Chadema kinawataka viongozi walioteuliwa na kiongozi mkuu huyo wa nchi kuondoa hofu katika utendaji wao wa kazi ili waweze kutekeleza shughuli za maendeleo wanazozisimamia.
Akizungumza katika mkutano huo, Diwani wa Ngarenano (Chadema), Isaya Doita amesema maendeleo katika jijini Arusha yanatokana na kazi nzuri ya baraza la madiwani la Chadema.
No comments:
Post a Comment