MHADHIRI wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) nchini Tanzania, Samson Mahimbo, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam akikabiliwa na shtaka la rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wa chuo hicho ili aweze kufaulu masomo yake.
Mhadhiri hiyo ambaye pia ni msaidizi wa kozi ya usimamizi wa barabara na usafirishaji, amefikishwa mahakamani leo Jumatano Agosti 14, 2019 na kusomewa shtaka linalomkabili.
Akimsomea hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi, Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Vera Ndeoya, amedai mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Januari 12, 2017.
Amedai siku ya tukio mshtakiwa akiwa katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Com David iliyopo eneo la Mlalakuwa, Mwenge, jijini Dar es Salaam, alitenda kosa hilo huku akiwa mwajiriwa NIT kama mhadhiri wa muhula wa kwanza 2015/2016.
Wakili Ndeoya alidai kuwa mshtakiwa huyo alitumia mamlaka hayo vibaya akiwa mhadhiri msaidizi wa kozi ya usimamizi wa barabara na usafirishaji yenye namba 07101 kwa kulazimisha rushwa ya ngono kutoka kwa mwanafunzi huyo kwa madai angemsaidia ufaulu kwenye masomo yake.
Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa alikana kosa hilo ambapo wakili Ndeoya amedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Shaidi amemtaka mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua na kitambulisho kutoka taasisi inayotambulika na atakayesaini bondi ya Sh. milioni moja.
Mshtakiwa amekidhi masharti ya dhamana na kuachiwa huru ambapo Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hivyo hadi Septemba 17,2019, itakapotajwa tena GPL
No comments:
Post a Comment