ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 15, 2019

Nyota Tanzanite apata fursa ya kusomeshwa Ujerumani

By Majuto Omary

Dar es Salaam. Kampuni inayojishughulisha na mazoezi ya kisasa ya Bodystreet ya Ujerumani imetoa ofa ya masomo ya mwaka mmoja kwa mchezaji bora wa timu ya Taifa ya wanawake ya chini ya miaka 20 (Tanzanite) Enekia Kasonga kusoma na kucheza mpira nchini humo.

Ofa hiyo ilitangazwa wakati wa utambulisho rasmi wa kampuni hiyo nchini Tanzania na Muasisi wa kampuni hiyo, Matthias Lehner na Emma Lehner wakati wa ufunguzi wa tawi la Tanzania maeneo ya Morocco karibu na ofisi ya kampuni ya simu ya Airtel.

Lehner alisema kuwa wamefuatilia mashindano ya Cosafa na hasa timu ya Tanzania ilipokuwa inacheza na Afrika Kusini na kuvutiwa na aina ya uchezaji wa timu ya Tanzania.

Alisema kuwa waliangalia mechi ya Tanzanite na Afrika Kusini akiwa na mtoto wake, Sarah Lehner ambaye ni kipa wa kutumainiwa wa klabu ya FFC Wacker Munichen ya Ujerumani na kuvutiwa na timu ya Tanzania.

Alifafanua kuwa tokea hapo wakaanza kufuatilia timu hiyo mpaka kushinda fainali ya mashindano hayo.

“Tumevutiwa na timu na kuamua kutoa ofa hiyo kwa mchezaji ambaye mbali ya kusoma mwaka mmoja, pia atapata fursa ya kucheza soka mjini Munichen kwa gharama zao,” alisema Lehner.

Alisema kuwa mbali ya kusoma, pia mchezaji huyo anaweza kufanya kazi na wao kwani pia atafundishwa jinsi ya kufanyisha mazoezi ya kisasa ya utimamu wa mwili, aina za rishe kwa afya na masuala mengine.

“Tunamshukuru mwanariadha nyota nchini, Filbert Bayi kwa kutupokea. Bayi aliwahi kukutana na mke wangu, Emma Lehner wakati akiwa anashiriki katika riadha na kuamua kumtumia katika suala hili,” alisema.

Kwa upande wale, Bayi alisema kuwa ni fursa kwa mchezaji huyo kuendeleza kipaji chake kwani uwepo wake Ujerumani itakuwa sifa kwa Tanzania.

“Nilimtafuta Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred kuhusiana na suala hili, hata hivyo simu yake haikupatikana na kuzungumza na Salum Madadi, hivyo mchakato mzima wa suala la ofa hii ya masomo na mafunzo itashughulikiwa na shirikisho hilo la mpira wa miguu,” alisema Bayi.

Bayi ambaye alizindua ofisi hiyo kwa kufanyishwa mazoezi, alisema kuwa kampuni ya Bodystreet imedhamiria kufanya mambo mengi ya maendeleo ya michezo nchini na kuanzia soka la wanawake.

No comments: