Kamanda wa polisi Mkoa wa Temeke, Amoni Kakwale
Kwa ufupi
By Fortune Franci, Mwananchi ffrancis@mwananchi.co.tz
Dar es salaam. Viongozi watatu wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha ACT Wazalendo na mwandishi wa habari mmoja wanaendelea kushikiliwa na Polisi nchini humo kwa tuhuma za kufanya maandamano bila kibali.
Wanaoshikiliwa ni pamoja na Mbarala Maharagande ambaye ni Katibu wa uadilifu, Mwikizu Mayama Mwenyekiti wa jimbo la Ilala, Haruna Mapunda mwandishi wa Gillybon na Saidi Mohammed Mwenyekiti wa chama hicho, Temeke.
Viongozi hao walikamatwa Jumamosi iliyopita ya Agosti 24, 2019 na jeshi la polisi wakati wakijiandaa kufanya mkutano wa ndani wa chama hicho Wilaya ya Temeke Dar es Salaam sambamba na ufunguzi wa matawi.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Agosti 26,2019, Wakili Bonifasia Mapunda amesema jana Jumapili jeshi la polisi liliwaeleza kuwa litawafikisha mahakamani lakini baada ya kufuatilia wameelezwa jalada liko kwa mwanasheria wa serikali.
"Nimefika hapa polisi Chang'ombe nimebahatika kuonana na mpelelezi amenieleza jalada liko kwa mwanasheria wa serikali hivyo mchana watawapeleka mahakamani" amesema Wakili Mapunda.
Amesema kama hawatapelekwa mahakamani au kuwapa dhamana atapeleka maombi Mahakama Kuu kutaka wafikishwe mahakamani au kupewa dhamana kwakuwa wameshikiliwa kinyume na sheria.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Temeke, Amoni Kakwale amesema hawezi kuzungumzia swala hilo kwakuwa ameshalitolea ufafanuzi.
"Swala hili nimeshalitolea ufafanuzi kama unataka ufafanuzi zaidi njoo ofisini," amesema kamanda Kakwale
Hata hivyo, jana Jumapili akizungumza na Mwananchi, Kakwale alisema viongozi hao wanashikiliwa na kuhojiwa kwa kosa la kufanya maandamano bila kuwa na kibali.
Katibu Mwenezi Mkoa wa chama hicho, Ray Matata amesema tayari yupo mwanasheria anayefuatilia swala hilo kisha atatoa taarifa zaidi.
"Jana polisi walisema watawafikisha mahakamani kakini hadi muda huu bado wanashikiliwa mwanasheria wetu anaendelea kufuatilia kisha tutawapa taarifa kama watawapa dhamana au kuwafikisha mahakamani" amesema Matata
Mkutano huo kabla ya kuzuiwa na kuamriwa kuondoka ulikuwa umeudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mshauri Mkuu wa chama hicho Maalim Seif pamoja na Katibu Mkuu Dorothy Semu.
No comments:
Post a Comment