ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 7, 2019

AFISA MANUNUZI, MZABUNI, KINAMPANDA WAKAMATWA KWA KUGHUSHI NYARAKA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimhoji Afisa Manunuzi wa Chuo cha Ualimu Kinampanda, Bw. Francis Muyombo (kushoto), kwa kukiuka taratibu za manunuzi ya Serikali na kughushi nyaraka, Oktoba 6.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua maktaba ya Chuo cha Ualimu Kinampanda, mkoani Singida, wakati akikagua ukarabati wa Chuo hicho Oktoba 6.2019.
  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua ukarabati wa Chuo cha Ualimu Kinampanda, mkoani Singida, Oktoba 6.2019.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua mlango, kwenye ukarabati wa Chuo cha Ualimu Kinampanda, mkoani Singida, na kutoridhishwa na vitasa hafifu vilivyotumika katika milango hiyo, Oktoba 6.2019.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Bw. Adili Elinipenda amkamate Afisa Manunuzi wa Chuo cha Ualimu Kinampanda, Bw. Francis Muyombo kwa kukiuka taratibu za manunuzi ya Serikali na kughushi nyaraka.

Pia alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, ACP Sweetbert Njewike amkamate na kumhoji Bw. Joseph Kisaka ambaye alikuwa mzabuni wa chuo hicho kwa kuwapatia (kusupply) vifaa ambavyo ni chini ya kiwango.

Alitoa agizo hilo jana jioni (Jumapili, Oktoba 6, 2019), wakati akikagua ukarabati wa majengo ya chuo hicho kilichopo wilayani Iramba, mkoani Singida ambako alibaini delivery note ikionesha kitasa kimoja kimenunuliwa kwa sh. 70,000 badala ya sh. 25,000.

Waziri Mkuu alisema quotation ya manunuzi inaonesha kwamba walipaswa kununua vitasa ambavyo vinafunga mara tatu (vya 3-level) lakini alipokwenda kukagua milango kwenye mabweni, ukumbi, na bwalo alikuta ni vitasa vya kufunga mara moja (vya 1-leavel).

“Serikali imetoa sh. bilioni 1.4 kwa kila chuo ili kufanya ukarabati wa vyuo vya elimu kikiwemo hiki cha kwenu. Ninyi mnanunua vifaa kinyume na utaratibu wa Serikali, hamvikagui, mnaweka tu vitu hafifu ambavyo havidumu. Haiwezekani!”

“Quotation yenu hapa inanionesha mlinunua vitasa 368 vya 3-level kwa gharama ya shilingi 70,000 kila kimoja. Lakini vitasa vilivyoko mlangoni ni vya 1-level ambavyo vinauzwa shilingi 25,000. Haya ni mabweni ya wanafunzi, wanaingi na kutoka kila wakati, ni kwa nini mnaweka vitu cheap wakati mnajua vitaharibika mapema? Maelekezo ya ununuzi wa Serikali yakoje?”

Alipoulizwa wametumia utaratibu gani kununua vifaa hivyo, Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Hamisi Njau alisema walikuwa wakitumia kamati ya manunuzi ambayo mwenyekiti wake alikuwa ni Makamu Mkuu wa Chuo na Katibu wake ni Afisa Manunuzi, Bw. Muyombo.

Bw. Muyombo alipoulizwa kama walikuwa wanayo BOQ ambayo ilikua ikiwaongozwa kufanya manunuzi, alijibu kwamba hawakuwa nayo bali alikuwa wakiorodhesha mahitaji yao na kuyapeleka kwa mhandisi.

Alipoambiwa aeleze tofauti ya vitasa vya 3-level na vya 1-level, Bw. Muyombo alijibu kwamba waliambiwa na mhandisi kwamba ndani ya kitasa kuna kibati ambacho kinatofautisha vitasa hivyo.

Waziri Mkuu alisema alisema Serikali inakataa udanganyifu kwenye manunuzi na haitavumilia watumishi wasiokuwa waaminifu. “Tena hili duka la huyo Kisaka ni la nguo wala siyo la hardware (vifaa vya ujenzi).”

Alimwambia Mkuu wa Chuo hicho alipaswa kusimamia ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati unaofanyika chuoni hapo.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa sh. 1,439.235,746 ili kukarabati chuo hicho kwenye maeneo ya utawala, maeneo ya kujifunzia, kumbi na mabweni ya wanachuo. Awamu ya kwanza ya fedha hizo iliingia Novemba, 2017 na awamu ya pili ikaingia Juni 2018.

Akizungumza na wanafunzi wa chuo hicho baada ya kufanya ukaguzi huo, Waziri Mkuu alisema Serikali inafanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini. “Mheshimiwa Rais alitoa sh. bilioni 1.4 kwa vyuo vyote ili kukarabati na kuboresha hadhi ya vyuo hivyo vikiwemo vya Monduli, Patandi, Kinampanda, Mtwara, Songea, Nachingwea, Korogwe, Kasulu na Butimba.”

“Nimeingia kwenye maktaba yenu nimeona bado vitabu vilivyopo ni vya muda mrefu, lakini kwa upande wa ajira bado tunaendelea kuajiri kwa awamu. Julai mwaka huu tuliajiri walimu 4670 na sasa hivi tumepata kibali cha kuajiri walimu 16,000,” alisema.

No comments: