Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametengua agizo la mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sofia Mjema aliyepiga marufuku ibada kufanyika katikati ya wiki.
Makonda ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba 22, 2019 baada ya kuulizwa na Mwananchi katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu kilichozungumzwa na Sofia baada ya video kusambaa mitandaoni ikimuonyesha mkuu huyo wa wilaya akipiga marufuku ibada kufanyika katikati ya wiki.
Katika video hiyo, Sofia amesema siku nyingine wananchi wa Ilala wanatakiwa kufanya kazi, “Tunajua kwenye kuomba Mungu ni mara tatu yaani Ijumaa, Jumamosi na Jumapili hizi siku nyingine marufuku nyinyi kazi mnafanya saa ngapi? Mnasema nimemuona mkombozi, unamuonaje bila kufanya kazi. Zunguka, ungezunguka mpaka kiama kama hufanyi kazi hazizunguki hizo.”
Katika maelezo yake leo, Makonda amesema, “Natengua kauli ya Sofia watu waendelee kwa imani zao bila kuathiri sheria za nchi. Viongozi tunapaswa kuwa makini tunapoingia kwenye masuala ya dini, dini ni imani.”
“Mimi ni mlokole huwezi kunipangia muda wa kusali. Tuwe na kiasi tunapoongelea imani za watu. Kuhamasisha watu kufanya kazi ni jambo jema ila lisiloingilia misingi ya imani nyingine.”
Makonda amewataka wakazi wa Ilala kuendelea kumuabudu Mungu, “wapo watu wanakula kupitia madhabahu, wanaamka asubuhi wanaombea wagonjwa, wanatusaidia kukemea mapepo, ulinzi na usalama unakuwepo. Hatuwezi kubeza kazi za viongozi wa dini. Ibada haina siku inahitaji moyo na utayari wa binadamu.”
Mkuu huyo wa Mkoa amesema inawezekana kuna mambo yanakwenda kinyume na taratibu, kumtaka Sofia kuwaita viongozi na kukaa nao.
No comments:
Post a Comment