Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt Ntuli Kapologwe akiwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mustapha Shaaban na viongozi wengine kutoka jumuiya ya Jamiyatul Akhlaaqul Islaam wakimsikiliza Mratibu Mkuu wa taasisi ya JAI, Athuman Massanga akielezea malengo ya taasisi yake katika kampeni ya kuchangia damu inayotarajiwa kufanyika kigoma kuanzia oktoba 24 hadi 27, 2019 katika viwanja vya Lake Tanganyika.
Baadhi ya waendesha baiskeli 18 kutoka mikoa mbalimbali wakiwa tayari kuanza safari ya kuelekea mkoani Kigoma kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuchangia damu salama. wanatarajia kufika kigoma tarehe 22 mwezi huu.
Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt Ntuli Kapologwe akikata utepe kuzindua msafara wa waendesha baiskeli 18 wanaoelekea mkoani Kigoma kuhamasisha uchangiaji damu.
Na Mathew Kwembe, Dodoma
Msafara wa waendesha baiskeli 18 kutoka Taasisi ya Kiislamu ya JAMIYATUL AKHLAAQUL ISLAAM (JAI) umeondoka leo mchana jijini Dodoma kuelekea mkoani Kigoma kwa ajili ya kuhamasisha kampeni ya taasisi hiyo ya kuchangia damu salama kwa ajili ya wagonjwa.
Kwa mujibu wa Mratibu wa kitaifa kutoka taasisi hiyo bwana Athumani Massanga, msafara huo unatarajia kuwasili mkoani Kigoma kuanzia tarehe 22 hadi 23 mwezi huu, tayari kwa ajili ya kushiriki kwenye kilele cha kampeni hiyo ya uchangiaji damu salama inayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Lake Tanganyika kuanzia tarehe 24 hadi 27 Oktoba 2019.
Amesema msafara huo wa waendesha baiskeli kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Lindi, Pwani, na Dar es salaam mbali na uhamasishaji kwa njia ya kuendesha baiskeli pia watafuatana na gari maalum ambalo litakuwa likihamasisha wananchi kuchangia damu, na kugawa vipeperushi kwa wananchi vinavyoelezea umuhimu zoezi hilo na kutangaza upendo na kutenda matendo mema kwa kusaidia wagonjwa.
Bwana Massanga amesema kuwa kila mwaka taasisi yake imekuwa ikiendesha kampeni ya kuchangia damu ambapo mwaka jana kilele cha kuchangia damu kilifanyika katika viwanja vya Maisara vilivyopo Zanzibar.
Amesema kampeni ya uchangiaji damu unafanyika mkoani kigoma kwani taasisi hiyo imejiwekea malengo ya kufanya kampeni ya uchangiaji damu katika mikoa mbalimbali nchini ambapo mwaka huu mkoa wa kigoma umebahatika kuwa mwenyeji wa kilele cha zoezi la kuchangia damu.
Zoezi kama hilo limewahi kufanyika katika mikoa ya Mwanza, Mara, Mbeya, Iringa, Mtwara, Lindi, Tanga na Kilimanjaro.
Mapema kabla ya kuzindua msafara huo wa waendesha baiskeli kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofiasi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo, Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt Ntuli Kapologwe amesema kuwa mahitaji ya damu ni makubwa kulinganisha na upatikanaji wake.
Amesema kwa kutambua juhudi za taasisi ya JAI, Serikali ya awamu ya tano inaunga mkono kampeni ya kuchangia damu ili kuwezesha wagonjwa waliopo katika hospitali na vituo vya afya nchini kupata huduma hiyo.
Amesema katika kuboresha huduma za sekta ya afya serikali ya awamu ya tano imejenga vituo 486 vya kutolea huduma za afya vikiwemo vituo vya afya 320 na hospitali za wilaya 67 nchin.
Amesema kuwa vituo hivyo vya kutolea huduma za afya nchini vitahitaji upatikanaji wa damu salama kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa husani akina mama wajawazito pindi wanapohitaji huduma hiyo.
Amesema kuwa serikali inaipongeza na kuishukuru taasisi hiyo kwa namna inavyojihusisha katika kusaidia jamii kwa njia ya kuhamasisha uchangiaji wa damu salama nchini ili kuwasaidia wagonjwa wasio kuwa na uwezo kwani hiyo ni katika utekelezaji wa amri ya upendo.
Aidha Dkt Kapologwe amesema kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo amechangia kiasi cha shilingi laki tano kwa taasisi hiyo na watumishi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi hiyo nao wamechangia shilingi laki tano kwa ajili ya kuwawezesha waendesha baiskeli hao waweze kununua maji na chakula wawapo safarini kuelekea mkoani Kigoma.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Sheikh Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Mustapha Shabani ambaye aliipongeza taasisi ya JAI kwa kuzingatia misingi ya dini ya Kiislam inayosisitiza upendo.
No comments:
Post a Comment