ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 15, 2019

TAASISI ZA UMMA NCHINI ZATAKIWA KUWAPATIA HUDUMA YA USAFIRI WATUMISHI WA UMMA WENYE ULEMAVU

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary M. Mwanjelwa (Mb) akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Amina S. Mollel Bungeni leo jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililohusu mpango wa Serikali wa kuwapatia huduma ya usafiri Watumishi wa Umma wenye Ulemavu.

Happiness Shayo-Dodoma
Tarehe 14 Novemba, 2019


Serikali imezitaka Taasisi za Umma nchini kuhakikisha zinatatua changamoto ya huduma ya usafiri kwa Watumishi wa Umma wenye Ulemavu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika wakati akijibu swali la Mhe. Amina S. Mollel (Mb) (Viti Maalum) aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwapatia huduma ya usafiri Watumishi wa Umma wenye Ulemavu.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, ili kufanikisha azma hiyo ya Serikali, Taasisi za Umma zinatakiwa kutekeleza miongozo inayotolewa ikiwa ni pamoja na Mwongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma Wenye Ulemavu wa mwaka 2008 unaoelekeza Waajiri kuwapatia huduma ya usafiri au kulipia gharama za mafuta ya kwenda na kurudi kazini kwa Watumishi wa Umma wenye Ulemavu ambao wana vyombo binafsi vya usafiri, lengo likiwa ni kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, Waajiri ambao hawatekelezi Mwongozo huo, wanakiuka maelekezo ya Serikali kwa kuwanyima stahiki watumishi wenye ulemavu, hivyo wakibainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi zilizopo.

Serikali kupitia Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini imejipanga kufanya Ufuatiliaji wa utekelezaji wa Mwongozo huo ili uweze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa amewakumbusha Waajiri kutoa kipaumbele cha mikopo ya vyombo vya usafiri kwa Watumishi wa Umma Wenye Ulemavu wanaokidhi vigezo vya kukopesheka ikiwa ni utekelezaji wa Waraka wa Watumishi wa Serikali Na.3 wenye Kumb.Na. C/AC.7/228/01/16 wa Juni 30, 2011 unaotoa Utaratibu wa Kukopesha Fedha Taslimu Watumishi wa Serikali kwa ajili ya kununulia Magari au Pikipiki pamoja na Matengenezo ya Magari na Pikipiki hizo.

No comments: