Dar es Salaam. Aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Ilala, Dk Makongoro Mahanga anatarajiwa kuzikwa Alhamisi Machi 26 katika makaburi ya Segerea jijini Dar es Salaam.
Dk Mahanga alifariki jana Jumatatu Machi 23 saa 12 alfajiri katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya kulazwa kwa siku mbili hospitalini hapo akipatiwa matibabu.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo nyumbani kwa marehemu, msemaji wa familia ambaye pia ni mjukuu wa Dk Mahanga, Dickson Juma amesema ripoti ya daktari amebainisha kwamba Dk Mahanga alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa pneumonia.
Amesema shughuli zote za mazishi zitaratibiwa nyumbani kwa marehemu ikiwa ni pamoja na ibada maalumu pamoja na kumuaga na anatarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Segerea.
"Mpaka sasa mwili bado uko mochwari Muhimbili lakini kesho utaletwa hapa nyumbani kwake, utalala hapa na Alhamisi ataagwa na kuzikwa hapa hapa Segerea," amesema Juma.
Dk Mahanga aliwahi kuwa mbunge wa Segerea na naibu waziri katika serikali ya awamu ya nne lakini baada ya kutoswa katika kura za maoni ndani ya CCM mwaka 2015, aliamua kuhamia Chadema.
Makada wa Chadema wamehudhuria msiba wa Dk Mahanga huku tahadhari za ugonjwa wa corona zikichukuliwa kwa kuweka maji ya kunawa mikono na kila mtu anayefika msibani hapo anatakiwa kunawa mikono.
Majirani na makada wa Chadema wamemuelezea Dk Mahanga kama mtu aliyependa kusimamia ukweli hata kama atakuwa peke yake. Wamesema watamkumbuka kwa ucheshi na mawazo yake ya kujenga demokrasia ya kweli.
"Ametusaidia sana kwenye chama chetu kwa kuhakikisha kwamba tunaendesha chama kwa kufuata misingi ya demokrasia. Alikuwa sio mtu wa kupinda pinda, kama umekosea atakwambia kwa uwazi," amesema kada wa Chadema, Francis Kisoli.
Kwa upande wake, Derrick Kato ambaye ni jirani wa Dk Mahanga amesema wamekuwa wakishirikiana na marehemu katika masuala mbalimbali hasa ya jumuiya na kikanisa.
No comments:
Post a Comment