Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na Mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Bibi Rozena Bilia Mwambogo alipomtembelea mnufaika huyo kijiji cha Mapogoro wilayani Chunya wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa mpango wa TASAF mkoani Mbeya.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na Mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Bibi Rozena Bilia Mwambogo wakielekea kushuhudia banda la nguruwe wanaofugwa na mnufaika huyo kutokana na ruzuku ya TASAF.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na mgonjwa, Mzee Gidison Mwayiyi ambae anauguzwa na mnufaika wa TASAF Bibi Rozena Mwambogo alipomtembelea mnufaika huyo katika kijiji cha Mapogoro wilayani Chunya wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa mpango wa TASAF mkoani Mbeya.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akimfariji mgonjwa, Mzee Gidison Mwayiyi ambae anauguzwa na mnufaika wa TASAF Bibi Rozena Mwambogo alipomtembelea mnufaika huyo katika kijiji cha Mapogoro wilayani Chunya.
Na. James K. Mwanamyoto – Chunya
Bibi mwenye umri wa miaka tisini, mkazi wa kijiji cha Mapogoro wilayani Chunya ambaye ni Mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) Rozina Bilia Mwambogo, ameboresha maisha yake kwa kujenga nyumba ya kuishi, kujishughulisha na kilimo na mazao ya chakula ikiwa ni pamoja na kufuga nguruwe.
Bibi Mwambogo ametoa ushuhuda wa kuboresha maisha yake kupitia TASAF wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wilayani Chunya yenye lengo la kukagua Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Mbeya.
Bibi Mwambogo amemueleza Dkt. Mwanjelwa kuwa, kabla ya kuingizwa kwenye mpango, hali ya maisha yake ilikuwa chini sana kwani hakuwa na kipato cha kumuwezesha kupata mahitaji muhimu ya kila siku kama chakula na mavazi.
Bibi Mwambogo ameongeza kuwa, malengo yake ya baadaye ni kuboresha zaidi maisha yake kwa kuongeza idadi ya Nguruwe na kuku na kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani hasa ya chakula.
Aidha, Bibi Mwambogo ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali wanyonge na kuwasaidia kupitia TASAF.
Kwa upande wake, Dkt. Mwajelwa amemueleza Bibi Mwambogo kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli inazijali na kuzithamini kaya zote maskini nchini ndio maana inatoa ruzuku kupitia TASAF, lengo likiwa ni kuzikwamua katika lindi la umaskini.
Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa, ziara yake ya kikazi ya kumtembelea Bibi Mwambogo ni sehemu ya kumuunga mkono Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amejipambanua kwa vitendo kuwajali wanyonge.
Dkt. Mwanjelwa amempongeza Bibi Mwambogo kwa kutumia vema ruzuku anayoipata licha ya umri mkubwa alio nao, na ametoa wito kwa wananchi hususani wanufaika wa TASAF kutumia vema fedha za miradi ya Serikali kama ilivyokusudiwa.
Uhawilishaji wa fedha kwa kaya maskini wilayani Chunya ulianza mwezi Julai, 2015 na hadi sasa awamu 23 za malipo zimefanyika ambapo kiasi cha shilingi 7,472,420,000/= za kitanzania kimetumika kuwapa walengwa ruzuku.
No comments:
Post a Comment