Moshi. Hatua ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuwaondoa baadhi ya wawakilishi wa vyama washirika katika baraza kivuli la mawaziri wiki iliyopita, inaonekana kuzidisha uwezekano wa kutokuwepo kwa umoja katika uchaguzi mkuu ujao, lakini vyama hivyo vimesema bado kuna dhamira.
Mwaka 2015, uchaguzi ulikuwa na ushindani mkubwa baada ya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliowapa fursa ya kusimamisha mgombea mmoja wa urais na pia katika majimbo na kata kadhaa.
Upinzani uliongeza idadi ya wabunge na madiwani.
Wakati huo, mchakato wa kuandika Katiba mpya ndio uliowaunganisha wapinzani na wajumbe kadhaa wa Bunge la Katiba waliosusia vikao na kuunda umoja huo waliouendeleza hadi katika Uchaguzi Mkuu.
Wakati umoja huo ukiwa umeshadhoofika kutokana na hamahama na timuatimua ndani ya vyama hivyo, na kukiwa hakuonekani hoja nyingine ya kuwaunganisha, Chadema ilifanya mabadiliko ya mawaziri wa kambi ya upinzani wiki iliyopita na katika baraza jipya hayumo mwenyekiti wa NCCR, James Mbatia, ambaye anaaminika kuwa alikuwa kiungo muhimu cha Ukawa.
Mbowe alinukuliwa akisema kuwa Mbatia alishamuomba asiwemo katika baraza hilo.
Mwingine ni mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF) ambaye alieleza katika ukurasa wake wa Facebook shukrani zake kwa Mbowe kwa kumuamini wakati wote, kitu kinachoonyesha anakubaliana na mabadiliko hayo.
Ikiwa imebakia takribani miezi saba kabla ya wananchi kupiga kura, wanachama wa vyama vya upinzani wakihamia NCCR-Mageuzi, uamuzi wa Chadema umezidisha sintofahamu ya uhusiano wa vyama hivyo ambavyo vilikutana Zanzibar na kueleza nia ya kushirikiana kuiong’oa CCM katika uchaguzi ujao.
“Hii Mbowe kuwaondoa NCCR na CUF kwenye baraza kivuli ni ishara wanaelekea kushindwa kabla ya uchaguzi. Hata CCM yenyewe inahitaji kura za wasio CCM. Bila ushirikiano hawafiki mbali,” alisema Askofu Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Dk Bagonza alisema kitendo cha Mbowe kuondoa vilivyokuwa vyama rafiki katika uchaguzi mkuu 2015 ni ishara mbaya.
Lakini mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii wa mjini Moshi, Conrad Kabewa alisema hali hiyo inatokana na viongozi wa upinzani kutoaminiana, jambo alilosema ni hatari.
“Ukitizama hili la Mbowe kumwondoa Mbatia lina kiini cha mazungumzo ya Mbatia na Rais Ikulu. Wale ambao hawakualikwa wanawaona walioalikwa kama wamesaliti upinzani,” alisema.
“Baadhi ya walioalikwa nao wanatoa kauli zisizoashiria kuungana na wasioalikwa. Hii peke yake inatosha kabisa kufuta hata chembe ndogo za kuaminiana zilizokuwepo wakati wakianzisha Ukawa.”
Hali ya kukosa ushirikiano katika uchaguzi ujao pia ilielezwa na Dk Richard Mbunda, mchambuzi wa siasa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Upinzani usijaribu kwenda katika uchaguzi ukiwa vipandevipande kwa kuwa hautapata matokeo mazuri hasa katika uchaguzi huu ambao CCM imejiimarisha sana,” alisema.
“Ukawa ulikuwa na manufaa sana kwa sababu ulijenga imani ya kisaikolojia kwa wapigakura na ile kugawana majimbo kuliwasaidia kutogawa kura. Pale walipogawana walianguka.”
Dk Mbunda alitoa mfano wa Jimbo la Segerea ambako mgombea wa CUF, Julius Mtatiro alipambana na mwenzie wa Ukawa kutoka Chadema na hivyo kuipa CCM ushindi rahisi.
Mchambuzi huyo alisema anachokiona bado kuna mvutano wa ndani kati ya NCCR-Mageuzi na Chadema hasa katika wakati huu ambapo NCCR-Mageuzi kinajitutumia kuonyesha kuwa ni chama hai.
Lakini katibu mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya alikuwa na mawazo tofauti kuhusu aina ya ushirikiano inayotakiwa baada ya Chadema kufanya mabadiliko hayo.
Sakaya alisema wana historia ndefu na Chadema katika suala la ushirikiano, akianzia mwaka 2005.
“Sisi CUF tulipokuwa na wabunge wengi tulikuwa tunashirikiana nao katika baraza la mawaziri kivuli bila tatizo. Matatizo yalianza mwaka 2010 wenzetu walipopata wabunge,” alisema mbunge huyo wa Kaliua.
Sakaya alikumbusha jinsi ambavyo Spika Anne Makinda aliporuhusu kuundwa kwa kambi ndogo ya upinzani isiyo rasmi baada ya CUF kutengwa na Chadema mwaka 2010.
CUF iligawanyika baada ya ushirikiano wa 2015; mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba akijivua nyadhifa zote hadi baada ya mwaka mmoja aliporejea na kutaka aendelee na nyadhifa zake, jambo lililosababisha suala hilo liende mahakamani na baadaye Maalim Seif na wafuasi wake kuhamia ACT-Wazalendo.
Baadhi ya wabunge wamekubali kuingia upande wa Profesa Lipumba huku wengine wakitarajiwa kutangaza msimamo baada ya Bunge kuvunjwa.
Pia, wachambuzi hao wanaangalia namna ambavyo Chadema inaweza kushirikiana na ACT-Wazalendo, ambayo haikuwapo katika umoja wa Ukawa.
ACT-Wazalendo inaongozwa na Zitto Kabwe, aliyeondoka kwa mgogoro Chadema, huku ikiwa na Maalim Seif Sharif, mwenyekiti ambaye aliunga mkono harakati za Ukawa 2015 wakati akiwa katibu mkuu CUF.
Pamoja na hali hiyo, bado viongozi wa baadhi ya vyama vya siasa wameshikilia kauli yao kuwa hatawaacha jitihada za kuunganisha nguvu na vyama vingine kwa ajili ya kuikabili CCM katika uchaguzi ujao, lakini wote wakisema umoja unataka vyama makini.
‘Matamanio ya wananchi’
Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema matamanio ya wananchi ni kuona “tunakwenda katika uchaguzi tukiwa kitu kimoja kama ilivyokuwa mwaka 2015 kwa baadhi ya vyama na sisi hatuko tayari kwenda kinyume na matamanio ya wananchi”.
“Tutashirikiana na vyama makini kwa baadhi ya mambo na mazungumzo yanaendelea ili kuona tunashirikiana kama kuachiana kata, ubunge na maeneo fulani fulani,” alisema Mrema ambaye pia ni katibu wa kamati ndogo ya kamati kuu ya Chadema ya mambo mtambuka, likiwamo la ushirikiano wa vyama.
Mwananchi lilipotaka kujua ni vyama gani na vingapi, Mrema alisema: “kwa sasa itoshe tu kusema tutashirikiana. Ni vyama gani vitafahamika baadaye lakini tayari ukiangalia huko nyuma tumekuwa tukishirikiana navyo kwa baadhi ya mambo, viongozi wetu walipowekwa ndani walikuwa wakiwatembelea na ushirikiano mwingine mwingine.
“Baadhi ya vyama vimeanza kuonyesha rangi zao kwa hiyo ni ngumu kushirikiana navyo. Tunataka kushirikiana na vyama makini,” alisema Mrema.
ACT Wazalendo
Naye Kabwe alisema ana imani muungano wa utakuwapo kwa kuwa viongozi wa juu wa baadhi ya vyama wapo katika mashauriano kuhusu mchakato huo.
“Hakuna njia yoyote ya kuitoa madarakani au kuishinda CCM pasipo muungano wa vyama. Mtu yeyote asijidanganye kuwa CCM itakiachia chama fulani jimbo, kama ilishindwa kukuachia uenyekiti wa serikali za mitaa kitakuachia jimbo?
“Jambo la msingi ni vyama hivi kuweka maslahi ya Taifa mbele, ingawa ni ngumu kufanya kwa sababu kila chama kina taratibu zake. Lakini katika ushirikiano kuna kupata na kukosa.”
Alisema ACT-Wazalendo ipo tayari kuungana na chama chochote makini ambacho kitakuwa tayari kupambana, akisema chama chake na Chadema ndivyo vyenye wajibu kuongoza ushirikiano huo.
“Endapo ushirikiano utakosekana, basi wa kulaumiwa ni ACT-Wazalendo na Chadema kwa sababu vina nafasi kubwa kwa sasa kuongoza vyama vingine katika ushirikiano,” alisema Zitto.
Azimio la ushirikiano
Kwa upande wake James Mbatia, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alisema moja ya maazimio ya mkutano mkuu wa Julai 27, 2019 ni ushirikiano na Halmashauri Kuu ilisisitiza jambo hilo.
Hata hivyo, alisema kinachokosekana sasa ni utashi wa kisiasa kuungana.
Mbatia alisema katiba ya NCCR-Mageuzi ibara ya 7(6) inatoa nafasi kwa chama hicho kushirikiana na vyama vingine vya siasa vyenye shabaha na malengo sawa, ikiwamo kushika utawala wa nchi.
“Hizo hatua za awali tulishazipitisha. Ushirikiano wa vyama unahitaji utashi wa kisiasa. Tofauti ya chama na chama itaendelea kuwepo na ndiyo maana kila chama kilisajiliwa kivyake,” alisema.
Alisema kuna mambo yenye maslahi kwa jamii ambayo inabidi kushirikiana.
“Sisi tuko tayari na tulishasema hadharani. Mimi niombe wenzangu tuangalie changamoto za Ukawa halafu tuone tunaendaje,” alisema.
Naye katibu mkuu wa CCK, Renatus Muabhi alisema kuna kutoaminiana, shaka na wasiwasi kutokana na mazungumzo yanayoendelea kati ya Rais na baadhi ya viongozi wa upinzani.
“Nafikiri kuna maneno mengi sana yanasemwa baada ya Mbatia kukutana na Rais na hata na Profesa Ibrahim Lipumba. Kuna shaka na kutoaminiana sasa kuliko 2015 baada ya hayo mazungumzo,” alisema.
No comments:
Post a Comment