Monday, April 6, 2020

Waliougua corona Tanzania wafika 24

By Mwandishi Wetu, Mwnanchi

Dar es Salaam. Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu ametangaza uwepo wa wagonjwa wengine wapya wanne wa maambukizi ya virusi vya corona nchini humo.
Waziri Ummy ametangaza leo Jumatatu Aprili 06, 2020 katika taarifa yake kwa vyombo vya habari inayoelezea mwenendo wa hali ya corona nchini
Amesema kuwa kati ya wagonjwa hao wanne, wawili wanatoka Tanzania Bara na wawili wanatoka Zanzibar
“Wizara ya Afya imethibitisha kuwepo kwa kesi mpya nne za maambukizi ya virusi vya corona (COVI-19) zilizopatikana Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar na kufanya kuwepo kwa jumla ya kesi 24 zilizoripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huu nchini” imesema sehemu ya taarifa hiyo
Amesema kuwa wagonjwa hao wapya ni pamoja na wawili ambao walitolewa taarifa na waziri wa afya Zanzibar jana Jumapili
Taarifa hiyo imesema kuwa wagonjwa wawili wa Tanzania Bara wote ni wafanyabiashara na ni raia wa Tanzania ambapo mmoja ni mkazi wa Mwanza aliyewasili kutoka Dubai Machi 24 na mwingine mkazi wa Dar es Salaam.
Taarifa hiyo ya waziri Ummy imesema kuwa wagonjwa wote wako chini ya uangalizi wa wataalam wa afya katika vituo maalum vya tiba vya Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar huku wizara ikiendelea kuwafuatilia watu wa karibu waliowahi kukutana na hao wagonjwa.

No comments: