NYOTA wa zamani wa Malaga ya Hispania mwenye asili ya Tanzania, Patrick Mtiliga ambaye aliwahi kumdhibiti Cristiano Ronaldo pindi akiichezea Real Madrid, amewataka viongozi wa soka nchini kutumia nguvu kubwa katika soka la vijana.
Mtiliga ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa michezo wa klabu ya Boldklubben af 1893 iliyopo nchini Denmark, alisema kutumia njia ya mkato kuleta mafanikio ni kama kucheza mchezo wa kubashiri ‘betting’.
Alisema siku zote unapocheza mchezo wa kubashiri huwa na matokeo mawili, kufanikiwa au kufeli lakini mipango ya muda mrefu huwa na matokeo mazuri kwenye soka.
“Hili ni eneo langu,
nimeshuhudia vile ambavyo mataifa makubwa katika sehemu mbalimbali ambako nimecheza soka wakifanikiwa kupitia uwekezaji ambao ulifanywa miaka mingi nyuma. Huo ndio msingi wa soka la Ulaya.
“Ni bora kupoteza kila kitu kwa kuwekeza katika vijana. Natambua kuwa Afrika imebarikiwa vipaji vingi vya soka lakini nani anaviangalia na kuvilea? Kama wapo ni wachache tena katika mataifa makubwa.
“Endapo kungekuwa na vituo vya kutosha vyenye usimamizi wa wakufunzi wanaoendana na soka la vijana ingekuwa rahisi kuona mafanikio yake,” alisema.
Mtiliga aliyezaliwa Januari 28, 1981 kwenye mji wa Copenhagen, Denmark baba yake Patrick ni Mtanzania. Alianza kucheza soka kwenye klabu ya vijana ya
Boldklubben katika mji aliozaliwa.
Kufanya kwake vizuri kwenye kikosi hicho kulimfanya umri uliposogea wa kuanza kucheza soka la kulipwa kusajiliwa na Feyenoord Rotterdam, iliyokuwa Ligi Kuu Uholanzi ambayo ni maarufu kama Eredivisie mnamo 1999.
Akiwa kama beki wa kushoto Patrick alitolewa kwa mkopo kwenda Excelsior Rotterdam iliyokuwa madaraja ya chini kwa lengo la kwenda kupata uzoefu.
Agosti 2006, alijiunga na wapinzani wa Feyenoord, NAC Breda kwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza muda wowote. Kufanya kwake vizuri kuliishawishi timu hiyo kumuongeza miaka miwili.
Neema zaidi ilimshukia Patrick ambaye alipata dili la kujiunga na Malaga CF inayoshiriki Ligi Kuu Hispania, 2009, ambako Januari 24 mwaka uliofuata alimkaba Cristiano Ronaldo kwenye La Liga pale ambapo timu yake ilikutana na Real Madrid kabla ya kutundika daruga 2017.
No comments:
Post a Comment