Sunday, April 19, 2020

Pierre Liquid akutwa na corona

By Nasra Abdallah

MCHEKESHAJI Pierre Liquid maarufu kwa vibwagizo vya kama utabaki kileleni, mama nakufaa, amekutwa na corona.
Akizungumza leo Jumapili na Mwanaspoti, Pierre ambaye jina lake ni Peter Mollel, amesema amebaini kukutwa na ugonjwa huo juzi.
Akizungumza kwa njia ya simu Pierre amesema kwa sasa yupo hospitali ya Amana akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.
Akieleza namna alivyogundulika kuwa ana corona,amesema hii ni baada ya kwenda kupima wiki iliyopita hospitali ya Temeke.
"Nina bosi wangu wa karibu ambaye kapata ugonjwa huu na kwa kuwa mara nyingi tuko naye alinishauri na mimi nikapime kwa nia njema ili kama ninao nipate matibabu mapema na kuepuka kuwaambukiza wengine.
" Hivyo nilienda hospitali ya Temeke, wakanipima ndipo nilipokutwa ninao na kuletwa hapa Amana ambapo kwa sasa ni moja ya kituo cha wagonjwa,"amesema Pierre.
Alipoulizwa anadhani ni wapi kaupatia, amesema "Huu ugonjwa mimi nitakuwa nimembukizwa nikiwa baa hakuna sehemu nyingine kwa kuwa ndio maeneo yangu ya kujidai,".
Hata hivyo amewapongeza baadhi ya viongozi waliotoa tamko la kufungwa kwa baa na kueleza kuwa hatua hiyo ni nzuri kwa kuwa maeneo hayo watu kuwa makini kujikinga na ugonjwa huu ni ngumu na pia huusisha mikusanyiko ambapo mtu akiwa hajalewa anaweza kukaa mbali na watu lakini pombe zikishamuingia akili hiyo haitakuwepo tena.
Wito wake kwa wananchi ameshauri kuchukua tahadhari ikiwemo maelekezo kutoka kwa wataalam wa afya kama kunawa mikono na maji tiririka,kuvaa barakoa na kuongeza kuwa hata yeye kabla hajaupata ugonjwa huo alikuwa hauchukulii kwa uzito.
" Wananchi nawashauri mchukue tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu, kwani mimi pia nilikuwa nauchukulia kimasihara, lakini sasa hivi kama hivyo nimekuwa mtu wa kukaa ndani, kushinda na barakoa na kulala na barakoa, gambe silipati tena maisha ambayo sikuyazoea, hivyo kinga ni bora,"ameshauri Pierre.

No comments: