ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 28, 2020

Serikali yaagiza barakoa kuteketezwa kabla ya kutupwa


AVELINE KITOMARY DAR ES SALAAM, Mtanzania

Serikali kupitia Wizara ya Afya, imetoa wito kwa wananchi kuteketeza barakoa zao baada ya kumaliza matumizi yake na kuitupa sehemu salama ili kuepusha kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko hususan ugonjwa wa homa kali ya mapafu unayosababishwa na virusi vya corona.

Wito huo ametolewa na Mkuu wa Kitengo cha Maji na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Afya, Anyitike Mwakitalima wakati akitoa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusu kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo.

“Wale ambao mmevaa barakoa zile ambazo zinatakiwa kutupwa baada ya kutumika mkumbuke kuitoboa kabla ya kuitupa ili mtu mwingine asiweze kuiokota, kuisafisha na kuirudisha katika mzunguko,” amesema.

Amesema katika baadhi ya nchi imethibitika kuwa, mgonjwa mmoja wa corona anaweza kuambukiza mpaka watu kumi kwa wakati mmoja hii inatokana na mwingiliano uliopo baina ya watu, hivyo kutoa wito juu ya kuchukua tahadhari ya hali ya juu.

Aidha amesema kuwa kwa wale ambao wanatumia barakoa za kitambaa, kuhakikisha wanazibadilisha kila baada ya masaa manne ili kuepusha kupata magonjwa mengine huku akisisitiza kuwa ni muhimu kabla ya kuzivaa zifuliwe kwa maji na sabuni kisha zipigwe pasi ili kujiweka salama zaidi dhidi ya magonjwa.

No comments: